Kuswali kabla na baada ya wakati

Swali 14: Wale wanaoenda katika matembezi na kambi, ambazo mara nyingi zinakuwa katika wakati wa majira ya joto, wanakesha nyusiku mpaka masaa kadhaa kabla ya alfajiri, kisha baadaye wanalala mpaka wanakosa Fajr. Matokeo yake hawaamki isipokuwa baada ya Fajr, takriban 13.30, kisha wanaswali Fajr na Dhuhr. Ni ipi hukumu ya hilo? Baadhi yao wanajengea hoja ukali wa baridi na wengine wanajengea hoja kuchoka kwa sababu ya kukesha usiku.

Jibu: Hapana shaka kwamba swalah ndio nguzo ya pili ya Uislamu, ambayo Uislamu umejengeka juu yake. ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu umejengwa juu ya mambo matano: kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba.”[1]

Jengine ni kwamba swalah imefaradhishwa ndani ya nyakati maalum. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا

“Kwani hakika swalah kwa waumini ni fardhi iliyowekwa nyakati maalum.”[2]

Kwa hivyo swalah haisihi kabla wala baada ya wakati wake isipokuwa kukiwepo udhuru.

Kuhusu kuswali kabla ya wakati, haisihi kabisa. Hata kama mtu ataswali mtu hali ya kudhania kuwa wakati umekwishaingia kisha baadaye ikabainika kuwa bado haujaingia. Mtu huyu analazima kuiswali tena upya swalah yake baada ya kuingia wakati. Ile swalah ya kwanza itakuwa ni Sunnah.

Ama akiiswali baada ya kuingia wakati, ikiwa ni kutokana na udhuru unaokubalika kwa mujibu wa Shari´ah kama vile kusahau au kupitiwa na usingizi, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kupitikiwa na usingizi au akaisahau swalah, basi aiswali pale atapoikumbuka. Haina kafara nyingine isipokuwa hiyo.”[3]

Wakati mwingine alilala yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake na hawakuamshwa isipokuwa na mwangaza wa jua, wakalipa swalah ya Fajr[4].

Akiichelewesha nje ya wakati bila ya udhuru unaokubalika katika Shari´ah. Kwa sababu akiichelewesha ya wakati bila ya udhuru unaokubalika kwa mujibu wa Shari´ah amefanya kitendo kisichoafikiana na amri ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), na hivyo anarudishiwa mwenyewe. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yeyote atakayefanya kitendo kisichokuwa ndani yake amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[5]

Bi maana atarudishiwa mtendaji.

Kutokana na haya ni wajibu kwa wale ndugu wanaotoka kwenda safarini kumshukuru Allaah (Ta´ala) juu ya neema hii, kwa sababu amewajaalia kuwa katika ustawi, urahisi wa maisha na usalama. Watekeleza yale ambayo Allaah amewawajibishia, kukiwemo kuswali ndani ya wakati wake, ni mamoja Fajr au swalah nyenginezo. Haijuzu kwao kuchelewesha swalah mpaka nje ya wakati wake kwa hoja eti walikuwa wamelala. Kikawaida ni kwamba hawapewi udhuru kwa sababu daima wanaweza kuweka alamu ya kuwaamsha ndani ya wakati wake. Vilevile wanaweza kulala mapema ili waamke wakiwa na uchangamfu.

Kuhusu baridi, sio udhuru katika kuchelewesha swalah nje ya wakati wake. Hivi sasa vipo vinavoweza kuyapasha maji katika safari hizi. Kwa hivyo ni lazima kwao kuyapasha maji ili watawadhe kwayo. Ikiwa mtu atahitaji kuoga janaba na akawa hana kitu cha kumuwezesha kuyapasha maji na akachelea juu ya nafsi yake, basi katika hali hii atafanya Tayammum. Baadaye mchana kukisha joto basi ataoga. Haijuzu kwake kuchelewesha swalah nje ya wakati wake kutokan na nyudhuru kama hizi dhaifu. Kwa hivyo nasaha zangu kwa ndugu ambao wanatoka katika safari hizi wamche Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala),  waikhofu siku ya Hesabu na watambue kuwa watakutana na Allaah na hivyo awafanyie hesabu juu yale waliyoyatenda. Kama alivosema Allaah (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الْإِنسَانُ إِنَّكَ كَادِحٌ إِلَىٰ رَبِّكَ كَدْحًا فَمُلَاقِيهِ

“Ee mtu! Hakika wewe unajikusuru kwa bidii kumwendea Mola wako, basi utakutana Naye.”[6]

Tunawaombea kwa Allaah wao na sisi awaongoze na awawafikishe katika yale anayoyapenda na kuyaridhia.

[1] al-Bukhaariy (8) na Muslim (16).

[2] 04:103

[3] al-Bukhaariy (597) na Muslim (684).

[4] al-Bukhaariy (595).

[5] Muslim (1718).

[6] 84:6

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/23-26)
  • Imechapishwa: 24/03/2026