Swali: Baada ya Allaah kunineemesha kwa neema ya Tawhiyd katika nchi hii katika miaka mitatu iliyopita na kwa idhini ya Allaah baada ya kupata sehemu ya elimu yenye manufaa katika elimu ya Tawhiyd na ´ibaadah nyingine, ninatarajia kusafiri hivi karibuni kwenda nchi yangu na mahali nilipozaliwa. Kwa kawaida ya watu wa huko, wazazi, ndugu, wasichana wa ami na wasichana wa shangazi watakuja kunipokea. Nimekusudia baada ya kufika kuwalingania Tawhiyd jamaa wa karibu na watu wa eneo hilo kwa ujumla. Je, inajuzu kuwasalimia kwa kushikana mikono hawa jamaa zangu wa kike kama wasichana wa ami na wengine wakati wa kunipokea ilihali hawajui Tawhiyd sahihi au nisiwape mkono? Naogopa wakakataa ulingano wangu ilhali ndiyo msingi wa dini.

Jibu: Wajibu juu ya mwanafunzi ni kutoa yale aliyo nayo ya elimu na kuwalingania watu kwa Allaah katika nchi zinazohitaji hilo, khaswa ikiwa hakuna anayechukua nafasi yake. Anatakiwa kuwa na upole, huruma, maneno mazuri na mbinu njema katika kufikisha ulingano. Ikiwa watu wa nchi yake hawajui baadhi ya hukumu za Allaah, basi awafikie na awabainishie hukumu hizo na awaongoze hata kama baadhi yao watapata uzito, kwa sababu mila zinazopingana na Shari´ah haziruhusiwi kuheshimiwa. Mitume hawakupingwa isipokuwa kwa sababu ya mila zinazopingana na haki? Hivyo ni lazima kuwa na subira. Ikiwa hali ni hiyo, basi uwatangulie kabla hujasafiri: waandikie sasa, uwaambie kuwa katika mila za nchi yenu kuna mambo fulani na uwanasihi wayaache na wasiyafanye ili wajue hilo kabla hujafika. Utakapofika kwao, waeleze kabla ya kuwasalimia kwa mkono kwamba jambo hilo halijuzu na kwamba salamu inakuwa pasi na kupeana mkono. Hili ni kwa mabinamu zako na mfano wao. Ama kwa dada zako, mama zako wadogo na shangazi zako, hakuna ubaya. Hili linahusu wasio Mahram kama mabinamu zako na majirani wa kike. Unawasalimia, unauliza hali zao na unawakaribisha, lakini bila kushikana mikono. Imethibiti kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

“Mimi siwashiki mikono wanawake.”

Hapo ilikuwa wakati wanawake walipotaka kumpa mikono, alisema:

“Mimi siwashiki mikono wanawake.”

Pamoja na alivyokuwa amepewa imani, hekima na kinga. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Naapa kwa Allaah mkono wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) haujawahi kugusa mkono wa mwanamke kabisa. Alikuwa anachukua kiapo chao cha utii kwa maneno tu.”

Kwa hiyo muumini anatakiwa kumuiga Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na asitafute radhi za watu kwa jambo linalopingana na dini. Allaah humwongoza amtakaye na humpoteza amtakaye. Wewe tekeleza wajibu wako: wakikubali, wana ujira na wewe una ujira, na wakikataa, basi umetekeleza uliowajibika. Jukumu lako ni kufikisha tu, kama ilivyokuwa hali ya Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam).

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3424/حكم-مصافحة-الاجنبية-ترغيبا-في-الدعوة-الى-الله
  • Imechapishwa: 26/08/2026