Kunyanyua mikono katika du´aa ya Qunuut ni Sunnah?

Swali: Je, ni katika Sunnah kunyanyua mikono wakati wa du´aa ya Qunuut?

Jibu: Ndio, mtu kunyanyua mikono yake wakati wa du´aa ya Qunuut ni katika Sunnah. Hivo ndivyo ilivyothibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Qunuut yake pindi alipokuwa akikunuti katika swalah za faradhi kipindi cha majanga[1]. Vilevile imesihi kutoka kwa kiongozi wa waumini ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba alikuwa akinyanyua mikono yake katika Qunuut ya Witr[2]. Huyu ni mmoja wa viongozi waongofu ambao tumeamrishwa kuwafuata. Kwa hivyo kunyanyua mikono katika Qunuut ya Witr ni Sunnah. Ni mamoja kwa imamu, maamuma au anayeswali peke yake. Muda wote unaokunuti basi unatakiwa kunyanyua mikono yako.

[1] Ahmad (03/137).

[2] “Sunan” ya al-Bayhaqiy (03/41).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (14/136)
  • Imechapishwa: 18/06/2017