Kumwita Allaah ”Fundi” au ”Mtengenezaji”

Swali: Je, ni sahihi kutumia neno “fundi'” (الصَّانع) kwa Allaah?

Jibu: Kwa maana ya mtengenezaji wa ulimwengu; ikiwa ni kwa namna ya kuthibitisha na si kwa namna ya kwamba ni sifa Yake. Katika mazingira hayo mtu anaweza kusema ”fundi”. Hata hivyo bora zaidi ni mtu kusema Muumbaji, kwa sababu Shari´ah imetaja Muumbaji na pia imetaja kitendo cha utengenezaji:

صُنْعَ اللَّـهِ الَّذِي أَتْقَنَ كُلَّ شَيْءٍ

“Utengenezaji wa Allaah ambaye ametengeneza kwa umahiri kila kitu.”[1]

Lakini neno hatujui kuwa kumetajwa neno fundi. Lakini baadhi ya watu wametumia maneno haya kama vile wanavyosema ”Aliyepo” na ”Kitu” kwa namna ya kukanusha hoja. Linaweza kutumiwa pia kwa ajili ya kuibainishia akili. Allaah amewapa watu akili ili waelewe na kutambua yanayowanufaisha na yanayowadhuru. Kwa hivyo waja wanamjua – kwa manaa ya kwamba wanamnyenyekea Muweza wa ulimwengu huu na Mwenye kuusimamia. Katika maumbile ya mtu kuna kumtukuza Ambaye ameumba, anaendesha ulimwengu huu na akaweka ndani yake vitu vingi. Hivyo akili inakua na kuongezeka katika unyenyekevu na udhalili kwa Yule ambaye ameumba ulimwengu huu, huku ikielekea Kwake na kujishikamanisha Naye hadi maarifa yatimie. Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) wakaja kwa ajili ya kukamilisha maarifa haya, kuyaunga mkono, kuyaimarisha na kuyaeleza kwa undani ili mwanadamu mwenye akili na jini mwenye akili wawe na maarifa kamili zaidi kuhusu Muumba na Fundi wao, watekeleze haki Yake na waache mambo yanayomghadhibisha. Hakika nafsi za waja na akili zao zimeumbwa juu ya mambo haya – yaani juu ya unyenyekevu, udhalili na kujikurubisha kwa Yule mwenye mamlaka ya kuendesha, kutoa na kuzuia. Hivyo basi mwenye akili hunyenyekea kwa hili jambo, kwani hakuna mwingine isipokuwa Fundi wa ulimwengu huu, naye si mwengine ni Allaah, (Subhaanahu wa Ta’ala).

[1] 27:88

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/25046/معنى-وحكم-اطلاق-الصانع-على-الله-تعالى
  • Imechapishwa: 02/02/2025