Kujitetea kwa maasi eti dini ni nyepesi – Vitimbi vya shaytwaan

Swali: Baadhi ya familia hula pamoja, kwa mfano watu wa nyumba moja na ndugu kila mmoja ana mke wake ambapo wakala pamoja. Wanapoambiwa kwamba jambo hili halijuzu, basi wanajitetea kwa kusema kuwa dini ni nyepesi na si uzito na eti kuwatenganisha wake na ndugu ni uzito. Tunaomba kubainishiwa haki kwa dalili.

Jibu: Hili pia ni katika upambaji wa shaytwaan, wanapodai kuwa dini ni  nyepesi kisha wanahalalisha maasi. Huu ni msiba. Dini ni nyepesi katika yale ambayo Allaah amefanya kuwa mepesi, si katika kuhalalisha maasi. Dini ni nyepesi pale unapougua unaruhusiwa kula katika Ramadhaan, ukishindwa kusimama unaswali kwa kukaa na ukikosa maji unaswali kwa kufanya Tayammum. Hii ndio maana ya wepesi. Si maana ya wepesi kwamba ukitamani wanawake basi uwaangalie, ukae nao au ukae chemba nao, hapana. Wepesi uko katika kulinda mipaka ya Allaah, kuacha aliyoyaharamisha Allaah na kutekeleza aliyoyaamrisha Allaah. Huu ndio wepesi. Mtu akishindwa jambo fulani, basi Allaah humbadilishia jingine lililo jepesi zaidi katika Shari´ah Yake. Huo ni wepesi kutoka kwa Mola wetu (Subhaanahu wa Ta´ala). Ama kudai kuwa inaruhusiwa kufanya maasi, kufurahia mke wa ndugu yako, mke wa mjomba wako au mke wa jirani yako, hili ni jambo ovu, ni katika maovu na hupelekea uzinzi na machafu. Lakini watu wengi hawatambui wala hawafahamu. Haifai kwa mwanaume kula pamoja na mke wa ndugu yake au mke wa mjomba wake, kwa kuwa si Mahram wake. Bali wanawake wakae peke yao na wanaume wakae peke yao.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1907/ما-حكم-اختلاط-الاقارب-بدعوى-ان-الدين-يسر
  • Imechapishwa: 11/03/2026