Swali: Kama ulivyobainisha, ee muheshimiwa, na miongoni mwake ni kughushi katika mitihani. Naomba ufafanuzi wa hukumu ya Shari´ah katika jambo hilo pamoja na kunitajia dalili.

Jibu: Ghushi katika mitihani bila shaka ni jambo linaingia katika maana ya ujumla. Dalili ni maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Yeyote atakayetufanyia ghushi basi si katika sisi.”

Hivyo ndivyo alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ikiwa ghushi katika mauziano ni haramu, basi katika elimu vilevile. Kwa sababu mwanafunzi anahusishwa naye matumaini na hukumu, basi akighushi katika mitihani na majaribio yake, huenda akahesabiwa kuwa ni miongoni mwa wanazuoni ilihali si hivyo. Bali amepata vyeti kupitia khiyana, uwongo na kughushi. Kwa hivyo anajidhuru yeye mwenyewe na kuwadhuru wengine.

Wakati fulani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipita karibu na ghala la chakula, akaingiza mkono wake humo ambapo vidole vyake vikapatana na unyevunyevu. Akasema:

”Hii ni nini, ee muuza chakula?” Akasema: ”Kimepatwa na mvua, ee Mtume wa Allaah.” Ndipo akasema: ”Mbona hukukiweka juu ya chakula ili watu wakione? Yeyote atakayetufanyia ghushi basi si katika sisi.”

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/30122/ما-حكم-الغش-في-الامتحانات
  • Imechapishwa: 12/09/2025