Kuchelewesha swalah kwa ajili ya darsa

Swali: Katika fatwa yako iliyotangulia umesema kwamba inafaa kuchelewesha swalah mwanzoni mwa wakati wake kwa ajili ya kusikiliza programu “Nuur ´alaad-Darb”. Tunaomba utubainishie dalili?

Jibu: Kwa mujibu wa dalili ya Qur-aan na Sunnah sidhani kama ni jambo linalotatiza kufaa kuchelewesha swalah mwanzoni mwa wakati wake kwa ajili ya kusikiliza programu “Nuur ´alaad-Darb”. Dalili ya Qur-aan ni katika maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا

“Kwani hakika swalah kwa waumini ni fardhi iliyowekwa nyakati maalum.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amebainisha nyakati za swalah kuanzia wakati fulani hadi wakati fulani. Kwa hivyo yule mwenye kuiswali ndani ya nyakati hizo mbili basi ameiswali ndani ya wakati wake uliowekwa.

Kuhusiana na Sunnah, amesema ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa):

“Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa kuhusu nyakati za swalah. Akajibu: “Wakati wa Fajr ni muda wa kuwa haujaingia ukingo wa jua. Wakati wa swalah ya Dhuhr unaanza pale linapopondoka jua linapondoka kwenye kilele cha mbingu na unaendelea muda wa kuwa haijaingia ‘Aswr. Wakati wa swalah ya ´Aswr ni muda wa kuwa jua halijapiga manjano na kuzama ule ukingo wake. Wakati wa swalah ya Maghrib unaanza pale linapozama jua na unaendelea muda wa kuwa haujapotea msitari mwekundu. Wakati wa swalah ya ´Ishaa ni hadi nusu ya usiku.”[2]

Imepokelewa katika Hadiyth nyingine ya kwamba bwana mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akimuuliza nyakati za swalah, ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku ya kwanza akaswali mwanzoni mwa wakati na siku ya pili akaswali mwishoni mwa wakati na akasema:

“Wakati ni baina ya nyakati hizi mbili.”[3]

an-Nawawiy amesema:

“Inafaa kuichelewesha swalah mpaka mwisho wa wakati wake bila tofauti yoyote.”[4]

Kwa hivyo kwa mujibu wa Qur-aan, Sunnah na maneno ya wanazuoni inafaa kuchelewesha swalah mpaka mwisho wa wakati wake. Simjui yeyote aliyesema kuwa ni haramu kufanya hivo isipokuwa kukhofiwa kuwa swalah mwisoni mwa wakati wake haitoswaliwa kwa njia inayotakikana – katika hali hiyo haitofaa kwake kuichelewesha. Ikiwa inafaa kwa mujibu wa Qur-aan, Sunnah na kwa maneno ya wanazuoni kuchelewesha swalah bila ya sababu yoyote, basi kuna tatizo lipi mtu akasiliza programu ya “Nuur ´alaad-Darb”, akaidika na akaswali mwishoni mwa wakati wa swalah hiyo? Ndio, ikiwa inapelekea mtu kupitwa na jambo la wajibu kama vile kuswali swalah ya mkusanyiko, basi hapo haitofaa kudondosha wajibu huo kwa sababu ya kusikiliza programu “Nuur ´alaad-Darb”. Kwa sababu wajibu haudondoki kwa kitu ambacho hakilingani nacho katika umuhimu.

[1] 04:103

[2] Muslim (612).

[3] Muslim (614).

[4] al-Majmuu´ (3/58).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/29-30)
  • Imechapishwa: 24/03/2026