Swali: Ni ipi dhana sahihi ya kufaa na kulingana (الكفاءة) katika ndoa? Je, makusudio ya mema ya duniani ni mwanamke mwema?

Jibu: Kufaa katika suala hili ni katika dini na uhuru kwa mujibu wa wanazuoni. Haya ndio maoni sahihi zaidi yaliyosemwa, kama alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا ۚ إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ

“Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamme na mwanamke na tukakufanyeni kuwa mataifa na makabila ili mtambuane. Hakika aliye mbora zaidi miongoni mwenu mbele ya Allaah ni yule mwenye kumcha Allaah zaidi kati yenu.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah ameondoa kwenu kiburi cha zama za kabla ya kuja Uislamu na kujivunia mababu. Watu wote ni wana wa Aadam na Aadam ameumbwa kwa udongo. Hivyo  basi hakuna ubora wa mwarabu juu ya asiye mwarabu, wala wa asiye mwarabu juu ya mwarabu isipokuwa kwa kumcha Allaah.”

Hivyo haifai kwa muumini kujivunia nasaba yake, mali yake au mambo kama hayo. Mwarabu anafaa na kulingana na asiye mwarabu, na pia anafaa kwa aliyekuwa mtumwa kisha akaachwa huru. Ama ikiwa ni mtumwa bado yuko utumwani, hilo linaweza kumletea madhara mwanamke isipokuwa akijua na akakubali. Katika hali hiyo hakuna ubaya.

Lengo kuu ni dini, kwa sababu dini ndiyo inayoleta kheri na kuondoa shari:

إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ

“Hakika aliye mbora zaidi miongoni mwenu mbele ya Allaah ni yule mwenye kumcha Allaah zaidi kati yenu.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwozesha Faatwimah bint Qays – naye ni Quraysh – kwa mtumwa wake aliyeachwa huru Usaamah. Kwa maana Usaamah bin Zayd bin Haarithah. Baba yake Zayd alimuoa Zaynab bint Jahsh al-Asadiyyah, kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuoa baada yake. ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf – naye ni wa kabila la Zuhrah wa Quraysh – alimwozesha Bilaal al-Habashiy aliyeachwa huru ambapo akamuozesha dada yake wa kabila la Zuhrah. Abu Hudhayfah bin ´Utbah bin Rabiy´ah alimwozesha mtumwa wake aliyeachwa huru Saalim. Saalim aliyekuwa mtumwa wa Abu Hudhayfah aliyeachwa huru. Akamuozesha binti ya ndugu yake al-Waliyd bin ´Utbah ilihali ni miongoni mwa watu mashuhuri wa Quraysh.

Ninachotaka kusema ni kwamba mambo haya hayafai kwa wenye akili kuyazingatia kwa upande wa nasaba. Bali kuzingatia muhimu sana ni katika kufaa kwa dini na uongofu wa mume na mke. Ikiwa dini imesimama sawa, basi hilo ndilo linalotakiwa.

[1] 49:13

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3378/مفهوم-الكفاءة-في-النكاح
  • Imechapishwa: 15/09/2026