Kikosi cha waswaliji wamemkuta imamu katika Tashahhud ya mwisho

Swali: Ni kipi bora mtu akija na akamkuta imamu ameketi katika Tashahhud ya mwisho; ajiunge naye katika swalah au asubiri mpaka pale imamu atakapomaliza swalah yake?

Jibu: Ni lazima kwake kujiunga pamoja na imamu isipokuwa akiwa pamoja na kikosi cha wengine; katika hali hii akitaka atajiunga pamoja na imamu na akitaka wasubiri ili wafanye swalah ya mkusanyiko ya pili. Lakini akiwa ni mtu mmoja na hana pamoja naye mtu mwengine, basi ajiunge pamoja na imamu. Ameamrishwa kufanya hivo. Lakini wakiwa watu wawili, watatu au wanne, basi hali hii ndio inatakiwa kutazamwa vyema. Wanayo khiyari ya kujiunga pamoja na imamu wakaswali pamoja naye kisha walipe kile kilichowapita na wanayo khiyari ya kusubiri mpaka pale atakapotoa salamu kisha wafanye swalah nyingine ya mkusanyiko.

Lakini akiwa ameshaingia ndani ya swalah kisha akahisi kuja kwa kikosi cha watu, basi inafaa kwake akainuia swalah ya sunnah midhali muda wa swalah bado ni mpana. Baada ya hapo ataswali pamoja nao swalah ya faradhi. Lakini kama ameshatoa salamu basi amekwishamaliza faradhi kwa hiyo swalah ya kwanza.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Mutanawwi´ah (17)
  • Imechapishwa: 01/12/2020