Kigezo katika kufaa na kutofaa kutumia mali ya umma

Swali: Watu wengi wanachukulia wepesi kile kinachoitwa ”haki ya umma”, wakitumia magari ya idara za serikali kwa mambo binafsi, simu kazini kuwapigia jamaa walioko nje ya eneo na mfano wa hayo. Ni kipi kigezo cha jambo hili?

Jibu: Ni wajibu kwa mfanyakazi na mtumishi wa serikali kumcha Allaah na kutotumia kilicho mikononi mwake isipokuwa kwa yale ambayo dola imeyahalalisha na kuruhusu. Iwapo kitu anachofanya kimeruhusiwa kwake, basi hapana vibaya. Vinginevyo, basi ajihadhari. Akiwa na shaka, basi ajiepushe na aache kilicho na shaka ndani yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Acha chenye kukutia shaka na kiendee kisichokutia shaka.”

Namna hii ndio amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

”Atakayejiepusha na mambo yenye shaka, basi atakuwa ameitakasa dini yake na heshima yake.”

Yale yaliyojulikana wazi kuwa wamemruhusu, basi hapana vibaya katika hilo. Waliyoyakataza ni lazima kuyaacha, kwa sababu kila muislamu ana jukumu la kusikia na kutii katika mema. Kwa hiyo chochote kilichokatazwa kwa mfanyakazi, asikifanye. Alichoruhusiwa, akifanye. Chenye kumtia shaka, basi akiepuke:

”Acha chenye kukutia shaka na kiendee kisichokutia shaka.”

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/30093/ما-حكم-استعمال-الحق-العام-لاغراض-شخصية
  • Imechapishwa: 07/09/2025