Je, madini yanayochimbwa ardhini yanatolewa zakaah?

Swali: Baadhi ya wanazuoni wamesema kuwa katika madini yanayochimbwa ardhini wapo wanaowajibisha zakaah ya mali kwa kiwango cha robo ya kumi (2.5%), na wengine wakasema hakuna chochote kilichowajibika. Ni lipi sahihi katika jambo hili?

Jibu: Sahihi ni kuwa hukumu yake hufanyiwa ufafanuzi. Madini ya dhahabu au fedha yanawajibika kulipiwa zakaah endapo yatabaki katika umiliki hadi yakatimiza mwaka. Madini yasiyokuwa dhahabu wala fedha, basi hukumu yake inafuata nia ya mwenye kuyatoa. Akiyatoa kwa ajili ya kunufaika nayo na kuyatumia, basi hakuna zakaah juu yake. Lakini akiyatoa kwa ajili ya biashara, basi yanakuwa kama mali ya biashara. Hivyo atalipa zakaah yake pindi yatakapofikisha mwaka. Yakikuwa dhahabu au fedha, basi anatoa zakaah mara tu yakitimiza mwaka. Ama madini kama chuma, shaba au mengineyo mfano wa hayo, basi yapo katika ufafanuzi huohuo. Akiyakusudia kwa biashara, basi yanakuwa mali ya biashara na anayatolea zakaah yanapokamilisha mwaka. Akikusudia kuyatumia binafsi kwa mahitaji yake, hakuna chochote kinachowajibika juu yake.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1094/هل-في-المعدن-زكاة
  • Imechapishwa: 24/01/2026