Je, inafaa kukataa tendo la ndoa kwa hoja ya kunyonyesha?

Swali: Je, inajuzu kuzuia mimba kwa sababu ya kunyonyesha kwa sababu akishika mimba basi maziwa yatakatika?

Jibu: Hili ni jambo kati ya mume na mke wake. Ikiwa mke ananyonyesha na wakakubaliana pamoja kuwa hatamuingilia kwa kuchelea kushika mimba, akatumia vidonge vya kuzuia mimba ili asishike mimba kwa ajili ya kubaki na maziwa ya kumnyonyesha mtoto na kumtunza, basi hakuna tatizo – Allaah akitaka. Kutumia vidonge vya kuzuia mimba kwa manufaa ya mtoto, kwa manufaa ya mama kwa sababu mimba itamdhuru au kwa sababu nyingine zenye uzito na ambazo hazina ubaya wowote, hakuna tatizo. Lakini kukataa kufanya tendo la ndoa, basi huenda jambo hili likawa na madhara kwa wanandoa na linaweza kuwapelekea katika shari kubwa kwa wote wawili. Huenda mwanaume akayaachia macho yake na hivyo akatumbukia katika machafu. Vivyo hivyo inapokuja kwa mke. Kwa hiyo kilicho bora zaidi ni kwamba amjamii, kisha atumie kinga inayozuia kushika mimba endapo wanaogopa mimba ambayo itadhuru mtoto aliye nao. Pia inawezekana mtoto akapewa maziwa mengine ya viwandani na akavunywa kutoka kifuani mwa mama yake iwapo wawili hao watakubaliana hivyo, basi hakuna tatizo. Ikiwa mume na mke watakubaliana kumwachisha mtoto kunyonya kutoka kwa mama yake na kumlisha maziwa mengine yaliyokaushwa au mengineyo, basi hakuna tatizo, kwa kuwa Allaah amesema:

فَإِنْ أَرَادَا فِصَالًا عَن تَرَاضٍ مِّنْهُمَا وَتَشَاوُرٍ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا

”Watakapotaka kumwachisha kunyonya kwa kuridhiana kati yao wawili na mashauriano, basi hakuna dhambi juu ya wawili hao.”[1]

[1] 02:233

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/30120/هل-يجوز-منع-الحمل-بسبب-الرضاع
  • Imechapishwa: 12/09/2025