Janaba kwa mwenye jeraha lenye bendeji

Swali: Ni ipi hukumu ya mtu ambaye amepata jeraha ambapo akafunga  juu yake bandeji, kisha akapatwa na janaba na daktari akamwamuru kuzuia maji yasifikie jeraha lote?

Jibu: Ikiwa mtu amepatwa na janaba kwa kuota au kwa kumjamii mke wake, naye ana jeraha lenye bandeji, basi aoshe sehemu nyingine za mwili wake na apake juu ya bandeji. Ataosha mwili wake wote kuhusu janaba isipokuwa jeraha, na bandeji iliyofungwa juu ya jeraha apake juu yake kwa kupitisha mkono ulio na maji juu yake, bila kuyafikisha maji kwenye jeraha. Ajitahidi kufanya hivyo. Ikiwa jeraha halina kitu juu yake au bandeji ni dhaifu kiasi kwamba maji yakiyafikia yatadhuru donda, basi atafanya Tayammum. Atakapomaliza kuoga na kukauka, apige udongo kwa mikono yake na apake uso wake na viganja vyake kwa nia ya sehemu ya jeraha. Ama ikiwa juu ya jeraha kuna bandeji au kifaa cha kulifunga, basi kupaka juu yake kunatosha. Vivyo hivyo yule mwenye plasta au kifaa cha tiba kwenye ubavu wake, mgongoni au tumboni kwa sababu ya ugonjwa, akipatwa na janaba, basi inatosha maji kupita juu ya plasta hiyo. Yakipita juu yake inatosha.

Swali: Je, atafanya Tayammum?

Jibu: Hatafanya Tayammum. Hana haja ya kufanya Tayammum. Kupaka juu kunatosha.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1422/كيف-يتطهر-الجنب-المصاب-بجرح-يتاثر-بالماء
  • Imechapishwa: 13/12/2025