Swali: Kuna mtu ambaye si msomi; hajui kuandika wala kusoma na anasema “Hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah” lakini hata hivyo anatawassul kwa asiyekuwa Allaah na anasema ”Ee al-Badawiy na al-Husayn! Naomba msaada” au anaweka nadhiri kwa asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall) na anayapapasa makaburi na ametumbukia katika shirki kubwa na si ndogo. Je, inajuzu kwetu kusema kuwa ni mshirikina au tuseme kuwa ni mjinga asiyejua Tawhiyd na tusimhukumu kufuru? Je, inajuzu kuswali nyuma yake, kumuozesha na kula kichinjwa chake kwa sababu anamtaja Allaah kabla ya kuchinja?

Jibu: Kumuomba asiyekuwa Allaah ni shirki kubwa. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote yule anayeomba pamoja na Allaah mungu mwengine hana ushahidi wa wazi wa hilo; basi hakika hesabu yake iko kwa Mola wake. Hakika hawafaulu makafiri.” (23:117)

وَلَا تَدْعُ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ ۖ فَإِن فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِّنَ الظَّالِمِينَ

“Wala usiombe badala ya Allaah asiyekufaa [ukimwabudu] na wala asiyekudhuru [usipomwabudu]. Na ukifanya hivyo, basi hakika utakuwa miongoni mwa madhalimu.” (10:106)

Tawassul kuna ambayo ni shirki, haramu na nyingine Bid´ah. Zote hizi zimekatazwa.

Kuhusiana na kupapasa makaburi kuna aina ya haramu na shirki. Mwenye kutumbukia katika kitu katika shirki inatakiwa kumbainishia hukumu na dalili. Akitubu na kurejea himdi zote ni za Allaah. Na akiendelea katika shirki alizomo atafanyiwa Takfiyr. Hivyo itakuwa haijuzu kuswali nyuma ya mshirikina, kumuozesha na kula kichinjwa chake hata kama atataja Jina la Allaah.

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (01/81)
  • Imechapishwa: 06/10/2020