Swali: Ni ipi hukumu ya mwenye janaba kugusa na kusoma Qur-aan?

Jibu: Hakuna vibaya kwake kwa kufanya yote mawili – Allaah akitaka. Kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

لَّا يَمَسُّهُ إِلَّا الْمُطَهَّرُونَ

“Haigusi isipokuwa waliotakaswa kabisa.”[1]

wanakusudiwa Malaika. Kungelikusudiwa watu, basi kungelikuja “wanaojitakasa”. Hivo ndivo alivosema Imaam Maalik kuhusiana na Aayah:

بِأَيْدِي سَفَرَةٍ كِرَامٍ بَرَرَةٍ

”Katika mikono ya Malaika waandishi. Watukufu, watiifu.”[2]

Wanaokusudiwa ni Malaika. Kama alivosema Allaah (´Azz wa Jall):

وَمَا تَنَزَّلَتْ بِهِ الشَّيَاطِينُ وَمَا يَنبَغِي لَهُمْ وَمَا يَسْتَطِيعُونَ  إِنَّهُمْ عَنِ السَّمْعِ لَمَعْزُولُونَ

”Hawakuteremka nayo mashaytwaan na wala haipasi kwao na wala hawawezi – hakika wao bila shaka wametengwa mbali kuisikiliza.”[3]

Kuhusu Hadiyth inayosema “Hakuna anayeigusa Qur-aan isipokuwa aliye msafi”, haikuthibiti licha kusimuliwa kwake kupitia njia nyingi. Imesimuliwa kupitia kwa ´Amr bin Hayy. Maoni sahihi zaidi ni kwamba kuna Swahabah anayekosekana katika cheni ya wapokezi. Imesimuliwa pia kupitia kwa Hakiym bin Hizaam ambapo katika cheni ya wapokezi yumo Suwayd Abu Haatim. Kuna maoni tofauti juu yake, lakini maoni yenye nguvu ni kwamba ni mnyonge. Hadiyth nyingine inayosema:

“Hakika muumini hanajisiki.”

Ameipokea at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Kabiyr” kupitia kwa Ibn ´Umar.  Hata hivyo sio hoja, ingelikuwa ni hoja, basi ingelikuwa na maana kwamba hakuna anayeigusa isipokuwa muislamu tu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kusafiri na Qur-aan kwenda katika nchi ya maadui.

Kuhusu kusoma Qur-aan, ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitusomea Qur-aan muda wa kuwa alikuwa hana janaba.”[4]

Hata hivyo haya yamesimuliwa na ´Abdullaah bin Salamah al-Muraadiy. Mwanafunzi wake ´Amr bin Murrah amesema juu yake:

“Alikuwa akitusimulia mambo ambayo tunayatambua na mengine tusiyoyatambua.”

[1] 56:79

[2] 80:15-16

[3] 26:210-212

[4] at-Tirmidhiy (146) aliyesema kuwa Hadiyth ni nzuri na Swahiyh. Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (146).

  • Muhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Mu´aanid, uk. 315
  • Imechapishwa: 13/07/2025