Imaam Muhammad bin Idriys ash-Shaafi´iy

Muhammad bin Idriys bin al-´Abbaas bin ´Uthmaan bin Shaafiy´ bin as-Saa-ib bin ´Ubayd bin ´Abd Yaziyd bin Haashim bin ´Abdil-Muttwalib bin ´Abd Manaaf bin Qusayy bin Kilaab bin Murrah bin Ka´b bin Lu-ayy bin Ghaalib. Imamu, mwanachuoni wa zama zake, mnusuraji wa Hadiyth na Faqiyh wa dini. Abu ´Abdillaah al-Qurashiy kisha al-Muttwalibiy ash-Shaafi´iy al-Makkiy al-Ghazziy. Anatokamana na ukoo wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na binamu yake. al-Muttwalib alikuwa ni kaka yake na Haashim ambaye na yeye alikuwa ni mtoto wa ´Abdul-Muttwalib.

Kuna maafikiano juu ya kwamba imamu alizaliwa Ghazzah. Baba yake Idriys alikufa akiwa bado kijana mdogo na Muhammad akachipuka hali ya kuwa ni yatima chini ya uangalizi wa mama yake. Akakhofia asije kupotea na hivyo akamtuma Makkah ambapo alikulia. Akaanza kujifunza kurusha mshale mpaka akawashinda marafiki zake. Kwenye mishale kumi alikuwa anapatia mishale tisa. Baada ya hapo akajishughulisha na lugha ya kiarabu na mashairi na akawa msitari wa mbele. Kisha akaanza kuipenda Fiqh na akawa mkubwa katika zama zake.

Alipokuwa takriban na miaka 20 akatoa fatwa na kuzingatiwa kwa haki zote kuwa imamu, akasafiri kwenda al-Madiynah na kusoma “al-Muwattwa’” chini ya Maalik bin Anas na akakisoma kutoka kwa hifdhi yake.

Akatunga tungo, akaandika elimu, akawarudi maimamu kwa mujibu wa mapokezi na akaandika misingi na matawi ya Fiqh. Sauti yake ikapea na wanafunzi wakamiminika kwake lukuki

Baadhi ya waliohadithia kutoka kwake ni pamoja na al-Humaydiy, Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Salaam, Ahmad bin Hanbal, Abu Thawr, Ishaaq bin Raahawayh, Ahmad bin Sinaan al-Qattwaan na wengineo.

Ibn ´Abdil-Hakam amesema:

“Wakati mama yake ash-Shaafi´iy aliposhika mimba, aliota jinsi sayari ya jupita inatoka nje ya uke wake mpaka alipofika Misri. Kisha kukaanguka katika kila mji kipande kutoka kwake. Wafasiri wa ndoto wakaifasiri ndoto kwamba mamake atazaa mwanachuoni ambaye alimu yake itawakhusu watu wa Misri, kisha baadaye itasambaa kwenye miji mbalimbali.”

al-Muzaniy amesema:

“Sijamuona mtu mrembo kama ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah). Wakati mwingine akizishika ndevu zake, basi hukutoki kitu.”

ar-Rabiy´ al-Mu-adhdhin ameeleza kuwa amemsikia ash-Shaafi´iy akisema:

“Nilikuwa nikifanya mazoezi sana ya kurusha mshale mpaka daktari akanambia: “Nachelea uje kupatwa na kiharusi cha joto kwa sababu ya kusimama kwako sana juani.”Kwenye kumi nilikuwa napatia tisa.”

´Amr bin Sawwaad amesema:

“ash-Shaafi´iy alinambia: “Hobi yangu mimi ilikuwa kurusha mshale na kutafuta elimu. Nikashikilia kweli kurusha mshale mpaka nikawa napatia kumi kwa kumi.”Akanyamaza kimya inapokuja katika elimu. Nikasema: “Naapa kwa Allaah kwamba wewe ni mkubwa zaidi katika elimu kuliko katika kurusha mshale.”

ar-Rabiy´ bin Sulaymaan amesema:

“ash-Shaafi´iy alizaliwa mwaka ambao alifariki Abu Haniyfah. Allaah awarehemu wote wawili.”

Abu ´Ubayd amesema:

“Sijawahi kumuona mtu mwenye akili zaidi kama ash-Shaafi´iy.”

Muslim bin Khaalid az-Zanjiy alimwambia ash-Shaafi´iy:

“Ee Abu ´Abdillaah! Toa fatwa! Naapa kwa Allaah kwamba naona kuwa una haki ya kufutu.”

Kipindi hicho alikuwa na miaka 15.

ash-Shaafi´iy amesema:

“Mtu kukutana na Allaah na dhambi zote mbali na shirki ni kheri kuliko kukutana Naye na kitu katika matamanio haya.”

ash-Shaafi´iy amesema:

“Laiti wangelijua ni matamanio gani yanayopatikana katika falsafa, basi wangeliikimbia kama wanavokimbia simba.”

Yuunus as-Sadaafiy amesema:

”Sijamuona mtu mwenye akili zaidi kama ash-Shaafi´iy. Siku moja nilihojiana naye juu ya masuala fulani kisha tukatengana. Baada ya muda fulani tukakutana akanishika mkono na kusema: ”Ee Abu Muusa! Hivi si sawa tuwe ndugu ijapo hatuafikiana katika suala fulani?”

Hili linafahamisha ukamilifu wa akili na uelewa wa imamu huyu –  mpaka hii leo wenye kuhojiana hutofautiana.

al-Ma´muun amesema:

”Nilimtahini ash-Shaafi´iy katika kila kitu nikamkuta ni mkamilifu.”

Ahmad bin Muhammad bin Bint ash-Shaafi´iy amesema:

”Nimemsikia baba na ami yangu akisema: ”Wakati Sufyaan bin ´Uyaynah alipokuwa akiulizwa tafsiyr au fatwa, anamgeukia ash-Shaafi´iy na anasema: ”Muulize huyu.”

Suwayd bin Sa´iyd amesema:

” Nilikuwa kwa Sufyaan wakati alipokuja ash-Shaafi´iy. Akatoa salamu na kuketi chini. Ibn ´Uyaynah akapokea Hadiyth inayotikisa moyo iliyomfanya ash-Shaafi´iy kuanguka chini na kupoteza fahamu. Kukasemwa: ”Ee Abu Muhammad! Muhammad bin Idriys amekufa.” Ndipo Ibn ´Uyaynah akasema: ”Ikiwa amekufa, basi itambulike kuwa amekufa mbora zaidi wa wakati wake.”

 ar-Rabiy´ amesema:

”Nilimsikia ash-Shaafi´iy akiulizwa kuhusu Qur-aan. Akasema: “Qur-aan ni maneno ya Allaah. Yeyote mwenye kusema kuwa imeumbwa basi amekufuru.”

Muhammad bin ´Abdillaah bin ´Abdil-Hakam amesema:

”Alikuwa ash-Shaafi´iy akichukia falsafa baada ya kujadiliana na Hafsw al-Fard. Alikuwa akisema: ”Naapa kwa Allaah bora kwa mwanachuoni kujadili na kusemwe: ”Mwanachuoni amekosea”kuliko azungumze falsafa na kusemwe: ”Zandiki.” Hakuna kitu kinachochukiza zaidi kwangu kama falsafa na wanafalsafa.”

Hii inafahamisha kwamba mfumo wa Abu ´Abdillaah ni kwamba kosa katika misingi si sawa na kosa katika mambo ya matawi ya ijtihaad.

ash-Shaafi´iy amesema:

”Makhaliyfah ni wanne: Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan, ´Aliy na ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz.”

Yahyaa al-Qattwaan amesema:

”Mimi namfanyia ash-Shaafi´iy maombi maalum.”

ash-Shaafi´iy amesema:

”Kusoma Hadiyth ni bora zaidi kuliko swalah za sunnah na kujifunza elimu ni bora kuliko swalah za sunnah.”

Yuunus amesema:

”Nilisema kumwambia ash-Shaafi´iy: ”Rafiki yetu al-Layth anasema: ”Endapo nitamuona mtu anayefuata matamanio anatembea juu ya maji, basi sintomkubalia.” Ndipo ash-Shaafi´iy akasema: ”Hakutosheleza. Laiti mimi nitamuona anatembea angani, basi sintomkubalia.”

´Uthmaan al-Antaamiy amesema:

”Nilikuwa nikitazama falsafa kabla ash-Shaafi´iy hajafika. Alipofika nikamwendea na kumuuliza suala fulani linalohusiana na falsafa. Akanambia. ”Unajua ni wapi ulipo?” Nikasema: ”Ndio, al-Fustwaat.” Akasema: ”Wewe uko Twaaraan.” ´Uthmaan akasema: “Twaaraan ni maeneo katika bahari ya Qulzum, ambapo hakuna sifa inayosalimika napo.”

Ahmad bin Hanbal amesema:

”ash-Shaafi´iy alikuwa mwenye kufuata upokezi pindi unapothibiti kwake. Sifa yake nzuri zaidi ilikuwa kwamba anapuuza falsafa. Hamu yake kubwa ilikuwa Fiqh.”

Husayn al-Karaabiysiy amesema:

“Siku moja ash-Shaafi´iy aliulizwa kitu kinachohusu falsafa ambapo akakasirika na kusema: “Muulize swali hili Hafsw al-Fard na marafiki zake – Allaah awatweze.”

ar-Rabiy´ amesema: “Nimemsikia ash-Shaafi´iy akisema:

“Natamani laiti watu watajifunza elimu hii pasi na kuninasibishia mimi chochote.”

az-Za´faraaniy amesema: “Nimemsikia ash-Shaafi´iy akisema:

“Hukumu yangu juu ya wanafalsafa naonelea wapigwe tawi la mitende na wabebwe juu ya ngamia na wazungushwe kati ya watu na kusemwe kwa sauti ya juu: “Haya ndio malipo ya mwenye kuacha Kitabu na Sunnah na akaiendea falsafa.”

´Abdur-Rahmaan al-Ash´ariy ameema: “Nimemsikia ash-Shafi´iy akisema:

“Madhehebu yangu juu ya wanafalsafa ni kwamba wabigwe bakora na watimuliwe nje ya mji.”

Haya yamepokelewa kwa mapokezi mengi kutoka kwa imamu huyu.

az-Za´faraaniy amesema: “Nimemsikia ash-Shaafi´iy akisema:

“Sijapatapo kujadili na yeyote juu ya falsafa isipokuwa mara moja tu. Na namwomba Allaah msamaha juu ya hilo.”

Imepokelewa kutoka kwa ar-Rabiy´ akisema: “Nimemsikia ash-Shaafi´iy akisema kuhusu mlango wa wasia:

“Lau mtu ataacha anausia vitabu vyake vya elimu kwa mwengine na katika vitabu hivyo kukaweko vitabu vya falsafa, basi vitabu hivyo havitoingia ndani ya wasia. Kwa sababu sio katika elimu.”

Abu Thawr amesema:

“Nilisema kumwambia ash-Shaafi´iy: “Andika kitabu kuhusu Irjaa´.” Akajibu: “Achana na jambo hilo. Ni kana kwamba alikuwa anatupilia mbali falsafa.”

Muhammad bin Ishaaq bin Khuzaymah amesema: ”Nimemsikia ar-Raabi´iy akisema:

”Wakati ash-Shaafi´iy alipojadiliana na Hafsw al-Fard ambapo Hafsw akasema: ”Qur-aan imeumbwa.” ash-Shaafi´iy akamwambia: ”Umemkufuru Allaah, Mtukufu.”

al-Muzaniy amesema:

”ash-Shaafi´iy alikuwa akikataza kujivugumiza ndani ya falsafa.”

Abu Haatim ar-Raaziy amesema: Yuunus ametuhadithia: Nimemsikia ash-Shaafi´iy akisema:

“Mama yake na al-Maariysiy alinambia: “Zungumza na Bishr akome juu ya falsafa.” Nikamzungumzisha na akaniita katika falsafa.”

al-Buwaytwiy amesema:

“Nilimuuliza ash-Shaafi´iy kuhusu kuswali nyuma ya Raafidhwiy?” Akasema: “Usiswali nyuma ya Raafidhwiy, Qadariy wala Murjiy.” Nikasema: “Tusifie nao.” Akasema: “Yule mwenye kusema kuwa imani ni kutamka peke yake ni Murjiy. Yule mwenye kusema Abu Bakr na ´Umar sio viongozi ni Raafidhwiy. Yule mwenye kujinasibishia matakwa kwake mwenyewe ni Qadariy.”

Ibn Abiy Haatim amesema: “Nimemsikia ar-Rabiy´ akisema: “ash-Shaafi´iy alinambia:

“Laiti ningelitaka kuandika kitabu dhidi ya kila anayekwenda kinyume basi ningefanya hivo. Lakini falsafa sio mambo yangu. Wala sipendi ninasibishiwe chochote katika hayo.”

Maneno haya matukufu yamepokelewa kwa njia tele kutoka kwa ash-Shaafi´iy.

ar-Rabiy´ amesema:

“Niliketi na ash-Shaafi´iy, ´Abdullaah bin ´Abdil-Hakam, Yuusuf bin ´Amr na Hafsw al-Fard. Hafsw akamuuliza ´Abdullaah: “Nini unachosema juu ya Qur-aan” lakini akagoma kumjibu. Kisha akamuuliza Yuusuf, lakini akagoma kumjibu. Hatimaye akamuuliza ash-Shaafi´iy ambaye akamshinda. Mjadala ukarefuka. Mwishowe ash-Shaafi´iy akaja na dalili juu ya kwamba Qur-aan ni maneno ya Allaah ambayo hayakuumbwa na juu ya ukafiri wa Hafsw.”

ar-Rabiy´ amesema:

“Nilikutana na Hafsw akasema: ”ash-Shaafi´iy alitaka kuniua.”

ar-Rabiy´ amesema:

”Nimemsikia ash-Shaafi´iy akisema: “Imani ni maneno na vitendo, inazidi na inashuka.”

Ahmad bin Hanbal amesema:

“ash-Shaafi´iy alisema: “Nyinyi ni wajuzi zaidi wa mapokezi yaliyo Swahiyh kuliko sisi. Hivyo basi upokezi ukiwa Swahiyh, basi nijuze ili niufanye kuwa maoni yangu, ni mamoja ni wenye kutoka al-Kuufah, al-Baswrah au Shaam.”

ash-Shaafi´iy amesema:

“Kila nitachokisema na wakati huohuo kikawa kinaenda kinyume na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi kichukueni na wala msinifuate kibubusa.”

ash-Shaafi´iy amesema:

“Mkipata kutoka katika kitabu change kitu kinachoenda kinyume na Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi kichukueni na muache yale niliyosema.”

ash-Shaafi´iy amesema:

“Kuna bwana mmoja alimuuliza: “Ee Abu ´Abdillaah! Hivi kweli utatendea kazi Hadiyth hii?” Ndipo akasema: ”Wakati wowote kutapokelewa Hadiyth Swahiyh kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na nisiitendee kazi, basi mtambue kuwa akili yangu imeondoka.”

ash-Shaafi´iy amesema:

“Ni mbingu ipi itanifunika na ni ardhi ipi itanibeba kukipokelewa Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na nisiifuate.”

ash-Shaafi´iy amesema:

”Hadiyth zote kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi ndio maoni yangu, ijapo hamtoisikia kutoka kwangu.”

Amesema tena:

”Itaposihi Hadiyth, basi hayo ndio maoni yangu. Itaposihi Hadiyth, basi yatupeni mbali maoni yangu.”

ar-Rabiy´ amesema:

”ash-Shaafi´iy alikuwa akiugawanya usiku sehemu tatu, theluthi ya mwanzo kisomo, ya pili anaswali na ya tatu analala.”

 ar-Rabiy´ amesema:

”ash-Shaafi´iy alikuwa akisoma Qur-aan nzima mara 60 wakati wa Ramadhaan.”

ash-Shaafi´iy amesema:

“Tangu nilipofikisha miaka 16 sikuwahi kula nikashiba isipokuwa mara moja tu ambapo niliingiza vidole vyangu kooni nikakitapika. Kwa sababu kushiba kunaufanya mwili kuwa mzito, moyo kuwa susuwavu, kunaondosha utambuzi, kunaleta usingizi na kunadhoofisha kufanya ´ibaadah.”

ash-Shaafi´iy amesema:

“Lazimiana na kuipa kisogo dunia. Kwani hakika kuipa nyongo dunia kunampendeza zaidi yule mwenye kufanya hivo kuliko mapambo ya mwanamke ambaye bado ni msichana.”

ash-Shaafi´iy amesema:

“Sijawahi kuapa kwa Allaah hali ya kuwa ni mwenye kuaminiwa wala kusema uongo.”

Ibraahiym bin Buraanah amesema:

“ash-Shaafi´iy alikuwa mwenye nguvu, mrefu na mtukufu.”

ash-Shaafi´iy amesema:

“Elimu ziko sampuli mbili; elimu ya dini, ambayo ni ile Fiqh, na elimu ya dunia, ambayo ni udaktari. Nyenginezo kama mashairi na mfano wake ni mambo yasiyokuwa na maana.”

ash-Shaafi´iy amesema:

”Kupotea kwa mwanachuoni ni yeye kuwa pasi na marafiki na kupotea kwa mjinga ni ule uchache wake wa akili na ambaye ni mpotevu zaidi kuliko wawili hao ni yule mwenye kutafuta rafiki asiyekuwa na akili.”

ash-Shaafi´iy amesema:

“Ukichelea kukwezeka kwa ajili ya matendo yako, basi jikumbushe nafsi yako ni radhi za nani unatafuta, ni neema gani unatamani na ni adhabu gani unaogopa. Yule mwenye kufikiria hivo basi atayadharau matendo yake.”

´Abdullaah bin Ahmad bin Hanbal amesema:

“Nilimwambia baba yangu: “ash-Shaafi´iy alikuwa ni mtu wa aina gani, kwa sababu nakusikia mara nyingi ukimuombea du´aa?” Akasema: “Ee mwanangu, alikuwa ni kama jua kwa ajili ya ulimwengu na uzima kwa watu.”

Qutaybah bin Sa´iyd amesema:

”ath-Thawriy amefariki na ndipo uchaji ukafariki, ash-Shaafi´iy amefariki na ndipo Sunnah ikafariki, Ahmad bin Hanbal amefariki na ndipo uzushi ukadhihiri.”

Abu Thawr al-Kalbiy amesema:

”Sijapatapo kuona mfano wa ash-Shaafi´iy na wala yeye mwenyewe hajapatapo kuona mfano wake mwenyewe.”

ash-Shaafi´iy amesema:

”Niliitwa ”Mnusuraji wa Sunnah” Baghdaad.”

Ahmad amesema:

“ash-Shaafi´iy alikuwa ni mtu mwenye ufaswaha zaidi.”

Abu Daawuud as-Sijistaaniy amesema:

“Sitambui kuwa ash-Shaafi´iy ana Hadiyth yenye kosa.”

´Abdul-Malik bin Haashim amesema:

“Mara nyingi tulikuwa tukikaa na ash-Shaafi´iy na hatukuwahi kumsikia na kosa la kisarufi.”

Ibn ´Abdil-Hakam amesema:

“Ukimuona ash-Shaafi´iy anavyojadiliana na wewe, basi utafikiri kuwa ni mnyama mkali anayekula. Hata hivyo yeye ndiye ambaye aliwafunza watu kuhoji.”

Haaruun bin Sa´iyd al-Ayliy amesema:

”Laiti ash-Shaafi´iy angejadiliana na wewe juu ya kwamba nguzo hii inatokana na mti, basi angekushinda kwa sababu ya nguvu yake katika kuhoji.”

Harmalah amesema:

”ash-Shaafi´iy aliulizwa juu ya mtu ambaye mdomoni mwake anayo tende na anasema: ”Nikiila, basi mke wangu ameachika, na nikiitema, basi mke wangu ameachika.” Aasema: ”Ameze nusu yake na ateme nusu yake.”

ash-Shaafi´iy amesema:

“Endapo wanachuoni wanaotenda kwa mujibu wa elimu yao sio mawalii wa Allaah, basi Allaah hana mawalii.”

Muhammad bin ´Abdillaah bin ´Abdil-Hakam amesema:

”Sijawahi kumuona mtu ambaye anatumia maji madogo kabisa na wakati huohuo anatawadha kikamilifu kama ash-Shaafi´iy.”

Abu Thawr amesema:

”Nimemsikia ash-Shaafi´iy akisema: “Mwanachuoni anatakikana kuweka mchanga kichwani mwake kama dalili ya kunyenyekea na kumshukuru Allaah.”

Ibn ´Abdil-Hakam amesema:

“Macho yangu hayajawahi kuona mtu mfano wa ash-Shaafi´iy. Nilifika al-Madiynah na nikaona namna ambavyo wafuasi wa ´Abdul-Malik al-Maajishuun wanavyochupa mpaka kwake wakisema: “Mwalimu wetu ambaye amemshinda ash-Shaafi´iy.” Nikakutana na ´Abdul-Malik na nikamuuliza juu ya suala Fulani. Akanijibu na nikamuuliza dalili. Akasema: ”Maalik anasema hivi na hivi.”Nikaiambia nafsi yangu: ”Ole wako. Nakuuliza dalili na wewe unanambia kuwa mwalimu wako anasema hivi na hivi.” Si vyenginevyo dalili iko dhidi yako na dhidi ya mwalimu wako.”

Harmalah amesema:

“Nimemsikia ash-Shaafi´iy akisema: “Watu walikuwa wakinitumia na kipindi hicho nilikuwa na miaka 13 na nilihifadhi “al-Muwattwa´” kabla hata sijabaleghe.”

 Harmalah amesema:

“Nimemsikia ash-Shaafi´iy akisema: “Natamani watu wajifunze elimu yote nilionayo ili nilipwe thawabu kwayo pasi na kupokonywa nazo.”

´Aliy al-Madiyniy amesema:

“Lazimianeni na vitabu vya ash-Shaafi´iy.”

Baadhi ya fani za imamu huyu ni tiba.

ash-Shaafi´iy amesema:

“Mwenye kula limau kisha akalala, basi kuna khatari kubwa akapata koo.”

 ash-Shaafi´iy amesema:

”Mtoto wangu wa kiume alikuwa katika hali mbaya kiasi cha kwamba hakuwa anaweza kuona mlango wa nyumba. Nikachukua mabaki ya maini na kumuweka machoni mwake na hivyo akawa mwenye kuona.”

 ash-Shaafi´iy amesema:

“Ni jambo la kushangaza kuona mtu anakula mayai yaliyochemshwa kisha akalala bila ya kufa.”

ar-Rabiy´ amesema:

“Nimemsikia ash-Shaafi´iy akisema: “Sijaona elimu ambayo ni tukufu zaidi baada ya elimu ya mambo ya halali na ya haramu kama ya tiba, lakini mayahudi na manaswara wametushinda kwayo.”

Harmalah amesema:

“ash-Shaafi´iy alikuwa akisitikishwa juu ya yale waliyopoteza waislamu katika mambo ya tiba na akisema: “Wamepoteza theluthi ya elimu na wakawaachia nayo mayahudi na manaswara.”

as-Saajiy amesema:

“Nilimwambia Abu Daawuud: “Ni nani maswahiba wa ash-Shaafi´iy?” Akasema: ”al-Humaydiy, Ahmad bin Hanbal na al-Buwaytwiy.”

al-Buwaytwiy amesema:

”Nimemsikia ash-Shaafi´iy akisema: “Lazimianeni na watu wa Hadiyth, kwani hakika katika watu wote wao ndio wenye kupatia zaidi.”

Yuunus bin ´Abdil-A´laa amesema:

“Nimemsikia ash-Shaafi´iy akisema: “Sijawahi kuona ambaye ni bingwa zaidi wa Fiqh na mkimya zaidi wa fatwa kama Sufyaan bin ´Uyaynah.”

Imaam Abu ´Abdillaah Muhammad bin Muhammad bin Muhammad bin Ghaanim amesema:

“ash-Shaafi´iy ni imamu katika lugha.”

al-Muzaniy amesema:

”Niliingia kwa ash-Shaafi´iy wakati alipokuwa katika hali ya kukata roho nikasema: “Ee Abu ´Abdillaah! Umeamkaje?” Akanyanyua kichwa chake na akasema: “Nimeamka hali ya kuwa ni mwenye kuiacha dunia, mwenye kutengana na marafiki zangu, mwenye kukutana na matendo yangu maovu, kupelekwa mbele ya Allaah na sijui kama roho yangu itaenda Peponi ili niipongeze au itaenda Motoni ili niipe pole.” Kisha kaanza kulia.”

Ahmad amesema:

“Nilimuuliza ash-Shaafi´iy juu ya kipimo ambapo akasema: “Wakati wa dharurah peke yake.”

Yuunus bin ´Abdil-A´laa amesema:

“Nimemsikia Abu ´Abdillaah ash-Shaafi´iy akisema baada ya kuulizwa kuhusu sifa za Allaah (Ta´ala) na kile anachoamini ambapo akasema: “Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) anayo majina na sifa zilizotajwa katika Kitabu Chake na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewaeleza nazo Ummah wake. Haitakiwi kwa kiumbe yeyote ambaye zimemfikia  kuzirudisha. Kwa sababu Qur-aan ndio imeteremka nazo na zimesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupitia wapokezi waaminifu. Yule mwenye kwenda kinyume nazo baada ya hoja kuthibiti kwake ni kafiri. Kabla ya kuthibiti hoja ni mwenye kupewa udhuru kwa ujinga kwa sababu utambuzi wa hayo hautambuliki kwa kutumia akili, uonekanaji wala kufikiria. Hatumkufurishi yeyote kwa ujinga isipokuwa baada ya kufikiwa na maelezo yake. Tunathibitisha sifa hizi na wakati huohuo tunakanusha ufanano. Hivo ndivo Alivyofanya Mwenyewe juu Yake:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

Musw´ab bin ´Abdillaah amesema:

“ash-Shaafi´iy alikuwa akikesha usiku kutwa na baba yake mpaka asubuhi.”

Yuunus bin ´Abdil-A´alaa amesema:

“Pindi ash-Shaafi´iy alipokuwa anaanza kuzungumzia tafsiri ya Qur-aan, ni kama kwamba ameshuhudilia uteremsho.”

al-Muzaniy au ar-Rabiy´ amesema:

“Tulikuwa kwa ash-Shaafi´iy siku moja ambayo alikuja mzee mmoja ambaye alikuwa amevaa nguo za pamba na bakora mkononi. ash-Shaafi´iy akasimama na akarekebisha nguo zake. Mzee yule akatoa salamu na kuketi chini. Mzee yule akasema: “Nina swali?” Akasema: “Uliza.” Akasema: “Ni ipi hoja katika dini ya Allaah?”Akajibu: ”Kitabu cha Allaah.” Akasema: ”Kisha nini?” Akajibu: ”Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Akasema: ”Kisha nini?” Akajibu: ”Makubaliano ya Ummah.” Mzee yule akasema: ”Ni wapi umetoa makubalino ya Ummah?” ash-Shaafi´iy akafikiria kitambo kidogo. Mzee yule akasema: ”Nakupa siku tatu.  Ima ulete dalili kutoka katika Kitabu cha Allaah au utubie kwa Allaah (Ta´ala).” Tahamaki ikabadilika rangi ya ash-Shaafi´iy. Halafu akaondoka zake na hakurudi isipokuwa katika ile siku ya tatu baina ya Dhuhr na ´Aswr. Akaketi chini na ghafla akaja yule mzee ambapo akatoa salamu na kuketi kitako. Halafu akasema: ”Umefanya?” ash-Shaafi´iy akasema: ”Ndio. Naomba ulinzi kwa Allaah dhidi ya shaytwaan aliyefukuzwa mbali na rehema Zake:

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

”Yule atakayempinga Mtume baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya waumini, Tutamgeuza alikogeukia na tutamuingiza Motoni – na ni uovu ulioje mahali pa kuishia!”[2]

”Hatomtupa Motoni kwa kule kwenda kinyume na njia ya waumini isipokuwa jambo hilo litakuwa ni faradhi.” Mzee akasema: ”Umesema kweli.” Kisha akashika njia na kuondoka zake. ash-Shaafi´iy akasema: ”Nimesoma Qur-aan kila siku mchana na usiku mara tatu mpaka nikaipata.”

az-Za´faraaniy amesema:

“ash-Shaafi´iy alitujia Baghdaad mwaka wa 195. Akabaki kwetu kwa miezi kadhaa. Halafu akaondoka zake. Alikuwa akijipaka hina na alikuwa na alikuwa na mabega mepesi.”

Ahmad bin Sinaan amesema:

“Nilimuona akiwa na nywele na ndevu nyekundu.”

Alikuwa akipaka rangi ya hina.

ash-Shaafi´iy amesema:

”Sijaona watu ambao wanashuhudia uongo kama Raafidhwah.”

ash-Shaafi´iy amesema:

“Elimu ni ile inayonufaisha na elimu sio ile iliohifadhiwa.”

ash-Shaafi´iy amesema:

”Laiti ningelijua kuwa maji ya baridi yanaipunguza heshima yangu, basi nisingeyanywa.”

Naapa kwa Allaah si wenye kulaumiwa kwa kumpenda imamu huyu, kwa sababu ni miongoni mwa wanamme wakamilifu katika zama zake. Allaah amrehemu – ijapo wako wengine tunaowapenda zaidi kuliko yeye.

[1] 42:11

[2] 04:115

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (10/5-99)
  • Imechapishwa: 04/01/2021