Ibn ´Uthaymiyn kuhusu viongozi wanaobadilisha Shari´ah kwa kanuni

Wale wanaohukumiana kwa kanuni na kuacha Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) sio waumini. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Naapa kwa Mola wako! Hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni hakimu katika yale wanayozozana kati yao kisha wasipate katika nyoyo zao uzito katika yale uliyohukumu na wajisalimishe kwa kujisalimisha.”[1]

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ

“Na yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio makafiri.”[2]

Watu hawa ambao wanahukumiana kwa kanuni kutokokana na matamanio na dhuluma, hawafanyi hivo katika nyanja maalum inayoenda kinyume na Qur-aan na Sunnah, lakini uhakika wa mambo ni kwamba wamebadili dini kwa kanuni hizi. Wamefanya kanuni hizi zikachukua nafasi ya Shari´ah ya Allaah. Hii ni kufuru. Hata kama wataswali, watafunga, watatoa swadaqah na kuhiji, ni makafiri. Midhali wameacha hukumu ya Allaah kwa kuijua na kuziendea kanuni hizi zinazokwenda kinyume na hukumu ya Allaah.

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Naapa kwa Mola wako! Hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni hakimu katika yale wanayozozana kati yao kisha wasipate katika nyoyo zao uzito katika yale uliyohukumu na wajisalimishe kwa kujisalimisha.”

Usistaajabu tukisema yule mwenye kubadilisha Shari´ah ya Allaah kwa kanuni ni kafiri hata kama ataswali na kufunga. Kukufuru baadhi ya Kitabu ni kukufuru Kitabu chote. Shari´ah haiko baadhi na baadhi. Ima uamini yote au ukufuru yote. Ukiamini sehemu yake na ukakufuru sehemu yake, wewe umeikufuru yote. Kwa sababu hali yako ni yenye kusema kuwa wewe unaamini tu yale yasiyopingana na matamanio yako. Kuhusu yale yanayopingana na matamanio yako huyaamini. Hii ndio kufuru. Kwa kufanya hivo utakuwa umefuata matamanio yako na kufanya ndio mungu wako.

Kwa kifupi ni kwamba masuala haya ni khatari sana. Haya ndio masuala ambayo ni khatari sana kwa watawala waislamu wa leo. Wameweka kanuni zinazoenda kinyume na Shari´ah na wao wanajua Shari´ah. Wameziweka kwa kuwaiga makafiri ambao ni maadui wa Allaah. Hawa ndio wametunga kanuni hizi na kuzifuata.

La ajabu kutokana na upungufu wa dini ya watu hawa na udhaifu wa dini yao wanajua fika kuwa walioweka kanuni hizi ni kafiri fulani bin fulani katika wakati fulani hapo kale miaka mia ya nyuma. Kafiri huyo yuko katika jamii inayotofautiana na jamii ya Kiislamu na wananchi wanaotofautiana na wananchi wa jamii ya Kiislamu. Pamoja na yote haya viongozi wanawawajibishia kanuni hizi waislamu na hawarejei katika Qur-aan wala Sunnah. Uislamu uko wapi? Imani iko wapi? Ukweli uko wapi juu ya ujumbe wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba ametumwa kwa watu wote? Ukweli uko wapi kuwa ujumbe wake ni wenye kuenea na unaendana na kila kitu?

[1] 4:65

[2] 05:44

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (02/261-262)
  • Imechapishwa: 01/12/2024