Ibn Baaz kuhusu nyama zinazotoka katika miji isiyokuwa ya waislamu

Swali: Tupeni fatwa kuhusu kuku na nyama zinazoingizwa kutoka nje? Je, fatwa zenu zimebadilika na ile iliyotajwa katika gazeti la ”Jaami´at-ul-Islaamiyyah” mwaka wa 95?

Jibu: Fatwa yetu siikumbuki ile ya gazeti, lakini fatwa yetu tunayoiendeleza ni kwamba msingi katika chakula cha watu wa Kitabu ni uhalali, kama Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) alivyosema. Allaah ametuhalalishia chakula cha watu wa Kitabu na ametuhalalishia kuwaoa wanawake wao wenye kujichunga na machafu. Hii ndio asili. Kwa hiyo vyovyote vile vilivyochinjwa na watu wa Kitabu miongoni mwa mayahudi na manaswara ni halali kwetu mpaka tujue kwamba hiki kitu maalum ni chenye kuharamishwa, kwa sababu kimechinjwa na asiyekuwa mfuasi wa Kitabu, kafiri mshirikina au kwa sababu kimechinjwa kinyume cha Shari´ah, kama kwa kunyongwa au mfano wake. Tusipolijua hilo na tukamkuta mnyama amechinjwa anayetoka katika nchi za manaswara au kutoka nchi za mayahudi, basi ni halali kwetu. Huu ndio msingi mpaka tujue kinyume chake. Hii ndiyo fatwa ninayoitoa kwa kufuata msingi huu.

Mwanafunzi: Kuhusu wao kutokata vichwa, bali humpitisha tu kwenye mashine?

Ibn Baaz: Ikiwa kitu kitapatikana bila kukatwa kichwa, basi hiyo inakuwa dalili kwamba kimenyongwa. Ama kile kinachoonekana kwa baadhi ya wachinjaji si hoja, kwa sababu wanakhitalifiana Ulaya na kwingineko. Wapo wanaochinja kwa kuchinja kwa mujibu wa Shari´ah, hata kwa kutumia mashine inayopita juu ya kuku na wengineo ikikata vichwa vyao. Kwa hiyo ikipita kwenye chombo chenye makali na vikakatwa vichwa inatosha, hata kama si kwa mkono wake mwenyewe. Muhimu ni kwamba vichwa vikikatwa kwa kitu chenye makali na damu ikamwagika, kama Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyosema:

”Kila kinachomwaga damu na kutajiwa jina la Allaah, kileni. Si kwa jino wala kwa ukucha.”

Kwa hiyo vichwa vikikatwa kwa kifaa chenye makali inatosha muda wa kuwa mchinjaji ni muislamu au mtu wa Kitabu.

Swali: Kutaja jina la Allaah si lazima?

Jibu: Kutaja jina la Allaah ni wajibu, lakini huenda wao wasilijue hilo au wakalihifadhi. Muislamu akiliacha kwa ujinga au kwa kusahau, kichinjwa chake kinakuwa halali. Vivyo hivyo mtu wa Kitabu akikiacha kwa kusahau au kwa ujinga, kichinjwa chake kinakuwa halali. Kama hatujui hali yake, kama vile kichinjwa cha muislamu. Anaweza kuchinja akasahau na akachinja hali hajui, anaweza kutotaja kwa kutojua. Msingi katika vichinjwa vya waislamu ni usalama. Vivyo hivyo vichinjwa vya watu wa Kitabu.

Swali: Kuna machinjio yaliyowasilishwa kwa baadhi ya waislamu kutaka kununuliwa na wakakuta mashine inayokata inafanya hivo katika ile hatua ya mwisho kabisa?

Jibu: Kwa hali yoyote ile msingi ni usalama. Yule aliyefahamu kuwa machinjio haya maalum hayapo sawa basi asinunue kutoka huko. Asipolijua hilo basi amesamehewa. Waislamu pia wamo wenye maasi na wamo wajinga, pamoja na hivyo tunakula vichinjwa vyao bila kuchunguza. Hatusemi kuwa tunaogopa huenda hakuchinja vizuri, hakutaja jina la Allaah na kadhalika. Tayari tumesema chakula wanachotukaribisha tunakila. Msingi ni kwamba ametaja na kwamba ni muislamu. Basi vivyo hivyo kuhusu watu wa Kitabu. Wala hairuhusiwi kutubana katika jambo ambalo Allaah amelifanya kuwa wasaa kwa watu wa Kitabu.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1083/حكم-اكل-الدجاج-المستورد
  • Imechapishwa: 15/02/2026