Swali: Je, mwanamke mwenye hedhi hana ruhusa ya kusoma Qur-aan?

Jibu: Kuna mitazamo tofauti kati ya wanazuoni. Shaykh Taqiyy-ud-Diin (Rahimahu Allaah) na kundi la wanazuoni wamesema ikiwa ataogopa kuisahau, basi atasoma, au ikiwa kusoma ni wajibu kwake kwa mujibu wa maoni mengine. Lililo karibu zaidi na usahihi – na Allaah anajua zaidi – ni kwamba anaruhusiwa kusoma, kwa sababu muda wa hedhi na damu ya uzazi ni mrefu. Si kama mwenye janaba ambaye muda wake ni mfupi. Mwanamke mwenye hedhi hawezi kulinganishwa na mwenye janaba. Kwa hivyo lililo karibu zaidi na usawa – na Allaah anajua zaidi – ni kwamba atasoma kwa kukariri kutoka kichwani. Aidha hayo ndio maoni yenye nguvu zaidi kwa mujibu wa dalili. Atasoma kutoka kichwani. Ikiwa kutahitajika kurudia kusoma kutoka ndani ya msahafu, basi asome akiwa amevaa glavu au kitu kingine kinachotenganisha na msahafu. Si sahihi mwanamke mwenye hedhi kumlinganisha na mwenye janaba, kwa sababu mwenye janaba muda wake ni mfupi. Anaweza kuoga na tatizo linaisha. Kwa hivyo kipimo hicho si sahihi katika jambo hili.

Ama Hadiyth isemayo:

“Mwanamke mwenye hedhi na mwenye janaba wasisome chochote katika Qur-aan.”

ni dhaifu. Kwa sababu ameipokea Ismaa´iyl bin ´Ayaash kutoka kwa Muusaa bin ´Uqbah. Ismaa´iyl anapopokea kutoka kwa wapokezi wa Hijaaz huwa dhaifu kwa mujibu wa wanazuoni wa Hadiyth. Isitoshe kipimo hicho ni batili.

Swali: Ikiwa ameruhusiwa kusoma Qur-aan, kwa nini asiruhusiwe kuigusa bila kifuniko?

Jibu: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kugusa msahafu kwa mwenye hadathi ndogo. Tusemeje kwa mwenye hadathi kubwa? Kugusa msahafu kumezuiliwa kwa mwenye hadathi ndogo, basi mwenye hadathi kubwa ni zaidi ya hapo.

Swali: Vipi kuhusu kile kinachopokelewa kutoka kwa Hudhayfah kwamba amemruhusu mwanamke mwenye hedhi na mwenye damu ya uzazi kusoma?

Jibu: Sikumbuki kitu kama hicho. Nasema sijui kitu kama hicho. Lakini kilicho sahihi ni kwamba inajuzu, kwa sababu kipimo cha kumlinganisha na mwenye janaba si sahihi. Aidha hakuna maandiko yanayomzuia kufanya hivyo. Isipokuwa ikiwa atahitaji kuugusa msahafu, basi afanye hivyo kwa kutumia kifuniko.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/31529/هل-للحاىض-ان-تقرا-القران-الكريم
  • Imechapishwa: 03/11/2025