Swali: Baadhi ya mapote ya Kiislamu yanafuata madhehebu ya Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) katika yale mambo wanayoafikiana naye. Lakini wakati huohuo katika mambo mengine hafuati madhehebu haya. Mfano wa mambo hayo ni kama kuomba du´aa za kwa pamoja na Maulidi. Je, mtu aseme kuwa watu sampuli hii ni Shaafi´iyyah katika Fiqh?

Jibu: Niliwaambieni kuwa wengi katika wafuasi wa madhehebu mane waliokuja nyuma wanayafuata katika Fiqh tu. Kuhusiana na ´Aqiydah hawafuati ´Aqiydah ya maimamu wa madhehebu haya. Unakuta ni Ash´ariyyah, Maaturiydiyyah na Mu´taziliyyah. Kwa ajili hii ndio maana utaona katika wasifu wake kumeandikwa ya kwamba madhehebu yake alikuwa ni Shaafi´iyyah, mwelekeo Shaadhiliyyah na kadhalika.

Mtu Shaafi´iy wa hakika ni yule anayefuata madhehebu ya Shaafi´iy katika Fiqh na ´Aqiydah. Huyu ndiye Shaafi´iy, Hanafiy, Maalikiy na Hanbaliy. Ni yule anayefuata mfumo wa imamu wake sawa katika ´Aqiydah na Fiqh. Kuhusiana na yule mwenye kufuata baadhi na akaacha mengine asinasibishwe na imamu anayemfuata.

Ni kweli kwamba ni wajibu kutofuata maoni yote ya imamu kibubusa. Ikiwa Ijtihaad yake inaenda kinyume na dalili haijuzu kwako kuichukua. Badala yake unatakiwa kuchukua yaliyo na dalili hata kama itakuwa kwa imamu mwingine usiyemfuata. Unatakiwa kuchukua yale yaliyo na dalili. Maimamu wenyewe wanausia haya. Shaafi´iy anasema:

“Itaposihi Hadiyth basi hayo ndio madhehebu yangu.”

Sehemu nyingine amesema:

“Maoni yangu yatapoenda kinyume na maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yachukue maneno ya Mtume wa Allaah na yatupilie mbali maneno yangu.”

Masuala hayahusiana na kufuata kichwa mchunga. Masuala yanahusiana na kuwa kati kwa kati katika mambo.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Qaa´idah Jaliylah fiyt-Tawassul wal-Wasiylah (10) http://alfawzan.af.org.sa/node/2125
  • Imechapishwa: 05/07/2020