Hukumu ya kutumia mali iliyochanganyika ya halali na haramu

Swali: Nina shaka kuhusu chanzo cha mali ya baba yangu na inawezekana anatumia humo pesa za ribaa na kughushi katika mauzo. Je, inajuzu katika hali hii kuchukua katika mali hiyo au kuoa kwa kutumia mali hiyo hali ya kuwa baba yangu ameridhia kunipa pesa na mimi ni mfanyakazi wa serikali lakini mshahara wangu hautoshi kuoa?

Jibu: Mali zilizochanganyika, kwa mujibu wa wanazuoni, inajuzu kuzitumia. Mali zilizochanganyika ambazo huenda ndani yake kukawa na haramu au kukawa na kitu chenye shubuha, mali hizo zinajuzu. Mali nyingi za watu ziko hivyo. Ni nani aliye salama kabisa? Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokea kodi kutoka kwa mayahudi na manaswara hali ya kuwa mali zao zilikuwa zimechanganyika; ndani yake kuna halali na haramu. Lalini ikiwa unajua kwa yakini kuwa mali hiyo hasa ni thamani ya sigara, thamani ya pombe, ni mali iliyoibiwa au iliyoporwa, basi usiichukue na si halali. Lakini maadamu mali hizo zimechanganyika na halali na isiyo halali, nawe hujui wala huwezi kutofautisha, basi msingi ni uhalali. Ni mamoja iwe ni mali kutoka katika mfuko wa waislamu, katika mali ya baba yako, ndugu yako au majirani zako. Ikiwa Allaah atakutosheleza bila hiyo nawe huna dharurah nayo na una kipato kilicho wazi na halali, basi jitosheleze kwa Allaah.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/2258/حكم-الاموال-المختلطة-من-الحلال-والحرام
  • Imechapishwa: 08/01/2026