Hukumu ya kumjamii mwanamke katika nifasi

Swali: Ni ipi hukumu ya kumjamii mwanamke katika damu ya uzazi? Damu ya uzazi una muda kiasi gani? Ni ipi hukumu ya mwenye kufanya hivo?

Jibu: Kumwingilia mwanamke katika nifasi ni haramu kama ilivyo katika hali ya hedhi. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ ۖ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ

“Wanakuuliza kuhusu hedhi. Sema: “Hiyo ni dhara, hivyo basi waepukeni wanawake katika hedhi. Wala msiwakaribie kujimai nao mpaka watwaharike.”[1]

Kuhusu muda wa damu ya uzazi inatofautiana. Baadhi ya wanawake muda wa damu yao ya uzazi inakuwa siku ishirini na wengine inakuwa chini ya hapo kiasi cha kwamba kuna wanawake ambao wanapata damu ya uzazi kwa muda wa siku tano kisha wanatwahirika. Baadhi ya wengine wanapitisha siku arubaini mpaka siku sitini. Kwa hivyo wanawake wanatofautiana.

Kuhusu ambaye amefanya hivo ni lazima kwake kutubu kwa Allaah kutokana na alichokifanya na asirudi. Allaah amemjaalia mambo yanayomwondoshea matamanio pasi na jimaa. Kwa mfano anaweza kumwingilia kati ya mapaja yake, anaweza kustarehe kwa kufanya punyeto kwa kutumia mkono wa mke wake. Kuna njia nyinginezo. Ama kumwingilia katika hali ya damu ya uzazi ni haramu. Lakini akitwahirika kabla ya siku arubaini ni halali kwake kumjamii? Ndio. Kwa sababu kama itafaa kwake kuswali basi jimaa itakuwa na haki zaidi ya kufaa.

Kuhusu yaliyopokelewa kutoka kwa baadhi ya Salaf kwamba mke wake alitwahirika kabla ya siku arubaini ambapo akamwacha, haya ni maoni yake. Lakini maoni sahihi yasiyokuwa na utatizi ndani yake ni kwamba yule ambaye imefaa kwake kuswali basi itafaa vilevile kumwingilia mke wake.

[1] 02:222

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (59) http://binothaimeen.net/content/1344
  • Imechapishwa: 02/07/2020