Kuhusu kuchinja kwa ajili ya maiti, ikiwa kwa mfano aliacha anausia juu ya theluthi ya mali aliyoacha, ikachukuliwa kutoka katika Waqf yake, basi ni wajibu kwa wasimamizi wa Waqf au wasia watekeleze wasia huo. Na ikiwa hakuacha wasia wala hakuacha Waqf lakini hata hivyo mtu akapendelea kumchinjia baba, mama yake au mtu mwengine, ni jambo zuri. Kitendo hicho kinazingatiwa ni kumtolea swadaqah maiti. Kumtolea swadaqah ni jambo linalokubalika kwa mujibu wa Shari´ah kwa mtazamo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

Ama kumtolea maiti swadaqah kwa ile thamani ya kichinjwa kwa kujengea ya kwamba ni bora kuliko kichinjwa chenyewe, ikiwa kichinjwa kiliwekwa katika Waqf au katika wasia, basi haitosihi kwa wakala huyo kubadilisha wasia huo na badala yake akatoa swadaqah thamani ya kichinjwa. Lakini ikiwa ni mtu mwengine tu ndiye ameamua kujitolea, hapo jambo ni jepesi. Ama mtu kuchinja Udhhiyah kwa ajili yake na kwa ajili ya familia yake, ni Sunnah iliyosisitizwa kwa ambaye ana uwezo juu ya jambo hilo. Kuchinja ndio bora kuliko kutoa swadaqah ile thamani yake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/16861/الاضحية-عن-الميت
  • Imechapishwa: 12/06/2024