Huu ndio mfumo wa Salaf. Mfumo huu umechukuliwa kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Usiulize ni wapi utachukua mfumo wa Salaf. Kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Qur-aan na Sunnah ndivyo vitavyokutambulisha mfumo wa Salaf.

Jengine ni kuwa usisome kutoka katika Qur-aan na Sunnah isipokuwa kupitia kwa wanazuoni waliobobea katika elimu. Ni jambo la lazima. Anayetaka kufuata mfumo wa Salaf basi ni lazima ashikamane na vidhibiti hivi vilivyowekwa katika Shari´ah. Vinginevyo kuna wengi leo wanaodai kuwa wanafuata mfumo wa Salaf ilihali wamo upotofuni na katika makosa makubwa. Pamoja na hivyo wanayanasibisha na ´Aqiydah ya Salaf. Ndio maana makafiri, wanafiki na wale nyoyo zao zina maradhi wakawa wanawatukana Salafiyyuun. Kila tendo la jinai, uharibifu na janga linalofanywa wanasema kuwa yamefanywa na Salafiyyuun. Salafiyyah haina lolote kabisa kuhusiana na haya. Mtu sampuli hii hafuati mfumo wa Salaf. Anafuata mfumo wa upotevu. Haijalishi kitu hata kama atajinasibisha na mfumo wa Salaf.

Ni lazima kwetu tutofautishe baina ya madai na uhalisia. Kwa sababu kuna wanaojiita bila ya uhakika. Huyu sio Salafiy na Salafiyyah haina lolote kuhusiana na yeye. Mfumo wa Salaf umejengwa juu ya elimu yenye manufaa, matendo mema, kujenga udugu kwa ajili ya Allaah na kushirikiana katika wema na uchaji Allaah. Huu ndio mfumo wa Salaf-us-Swaalih. Ni mfumo ambao mwenye kushikamana nao ameokoka na mitina na atapata radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

رَّضِيَ اللّهُ عَنْهُمْ وَرَضُواْ عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الأَنْهَارُ

“Allaah ameridhika nao na wao wameridhika Naye na Amewaandalia mabustani yapitayo chini yake Mito.”[1]

[1] 09:100

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: as-Salafiyyah haqiyqatuhaa wa simaatuhaa, uk. 34-36
  • Imechapishwa: 06/05/2024