Swali: Baadhi ya wanafunzi Ijtihaad zao zinawafikisha kwenda kinyume katika jambo ambalo linatambulika vyema katika dini. Je, mambo yanayotambulika vyema katika dini yanafanyiwa Ijtihaad?

Jibu: Kila kinachotambulika vyema katika dini kwa dalili za wazi kutoka katika Qur-aan na Sunnah au maafikiano ya Salaf basi Ijtihaad haina nafasi. Bali lililo la wajibu ni kuliamini, kulitendea kazi na kutupilia mbali kinachokwenda tofauti na maafikiano ya waislamu. Msingi huu mtukufu hauna tofauti kwa wanachuoni. Tofauti inakuwa katika mambo yenye tofauti ambayo dalili zake hazijakuwa wazi kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Katika hali hiyo yule ambaye atapatia, basi anapata thawabu mara mbili, na yule ambaye atakosea, basi anapata thawabu mara moja muda wa kuwa ni miongoni mwa wanachuoni anayestahiki kufanya Ijtihaad na wakati huohuo akatumia uwezo wake katika kutafuta haki hali ya kuwa ni mkweli na ni mwenye kumtakasia nia Allaah. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Akijitahidi hakimu na akapatia, basi ana ujira mara mbili, na akijitahidi na akakosea, basi ana ujira mara moja.”[1]

[1] Ameipokea al-Bukhaariy (7352) na Muslim (1716).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (07/45)