Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

188 – Mama wa waumini Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

(إنَّهُ يُسْتَعْمَلُ عَلَيْكُمْ أُمَرَاءُ فَتَعرِفُونَ وتُنْكِرُونَ، فَمَنْ كَرِهَ فَقَدْ بَرِئَ، وَمَنْ أنْكَرَ فَقَدْ سَلِمَ، وَلَكِنْ مَنْ رَضِيَ وَتَابَعَ)

.قَالوا: يَا رَسُول اللهِ، ألا نُقَاتِلهم؟ قَالَ: (لا، مَا أَقَامُوا فيكُمُ الصَّلاةَ)

“Mtaletewa watawala ambao kuna mambo mtayoyajua na mengine mtayachukia; yule atakayechukia basi ameokoka, na yule atakayekanya amesalimika, lakini yule atakayeridhia na kufuata [basi huyo ataangamia kama watavyoangamia].” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah, si tumpige vita?” Akasema: “Hapana, maadamu anasimamisha swalah.”[1]

Bi maana watawala hawa hawasimamishi adhabu za Allaah na hawasimami katika maamrisho ya Allaah. Hawa ni wale viongozi wa mtawala waliopewa ahadi.

Hapa kuna dalili yenye kuonesha kuwa mtawala yeyote pale tutapoona yale tunayoyachukia, inatakiwa kwetu kuyakemea na kuwakataza. Wakiongoka, ni kheri kwetu na kwao. Na ikiwa hawakuongoka, ni kheri kwetu na maovu kwao.

Haijuzu kuwapiga vita watawala ambao tunaona maovu kwao. Kwa sababu kunapatikana shari kubwa kwa kuwapiga vita na kupitwa na kheri nyingi. Kwa kuwa wakipigwa vita hilo halitowazidishia lolote zaidi ya shari. Wao ndio viongozi na hivyo wanajiona wako juu ya watu [wote]. Watu wakiwapinga na kuwapiga vita, shari yao inazidi. Isipokuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameweka sharti moja:

“… maadamu wanaswali.”

Hii ni dalili yenye kuonesha kuwa ikiwa hawaswali basi inatakiwa kwetu kuwapiga vita.

[1]Muslim (1854).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (02/435)
  • Imechapishwa: 18/08/2025