Hadiyth zimegawanyika katika mafungu makuu mane

Swali: Ninaposoma vitabu vya Sunnah napata kuwa kuna Hadiyth ambazo ni Swahiyh, dhaifu na zilizozuliwa. Je, inajuzu kuzitumia kama dalili na kuzitendea kazi?

Jibu: Sunnah, kama alivosema ndugu muulizaji, imegawanyika mafungu matatu:

1 – Swahiyh.

2 – Nzuri.

3 – Dhaifu.

4 – Zilizozuliwa.

Kuhusu Hadiyth ambazo ni Swahiyh na nzuri zinatumiwa kama dalili na kutendewa kazi. Namaanisha kutendea kazi zile hukumu zinazofahamishwa nazo na zile khabari zilizomo ndani yake zinatakiwa kusadikishwa.

Ama Hadiyth ambazo ni dhaifu ikiwa zinaungwa nguvu kutokana na wingi wa njia zake na zengine zinazoisapoti, basi Hadiyth hiyo inakuwa ni nzuri kutokana na zengine (حسناً لغيره) na inaungana na Hadiyth ambayo ni nzuri na hivyo inatumiwa kama hoja. Isipoungwa nguvu basi haitumiwi kama hoja. Lakini wako wanachuoni waliotumia kama ushahidi katika ubora wa matendo au kuonya yaliyokatazwa kwa sharti tatu:

Ya kwanza: Hadiyth hiyo iwe na msingi sahihi unaoweza kutegemewa.

Ya pili: Hadiyth hiyo isiwe ni dhaifu sana.

Ya tatu: Mtu asiitakidi usahihi wake kufika kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa msemo mwingine mtu asiamini kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye kasema hivo. Mfano wa hilo endapo kutapokelewa Hadiyth inayozungumzia ubora wa swalah ya mkusanyiko na Hadiyth hiyo ikawa ni dhaifu. Lakini hata hivyo Hadiyth hiyo imetimiza sharti hizi tatu tulizozitaja. Basi Hadiyth hiyo tunaweza kuitumia kama ushahidi. Kwa sababu swalah ya mkusanyiko ni wajibu na msingi wa ubora wake umethibiti. Hivyo kukitimia sharti hizi tatu basi katika hali hiyo msingi tayari upo. Kukipatikana sharti zengine mbili za mwisho – isiwe ni dhaifu sana na mtu asiitakidi usahihi wake kwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – basi itafaa kuitumia kama ushahidi.

Ama kuhusiana na Hadiyth zilizozuliwa haijuzu kuinasibisha kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa hali yoyote ile. Bali haijuzu hata kuiitaja. Isipokuwa kwa lengo la mtu kubainisha hali yake ili watu wasidanganyike nayo. Kadhalika Hadiyth ambayo ni dhaifu tuliyotaja punde haijuzu kuitaja isipokuwa kwa kuambatanisha kutaja udhaifu wake. Hata kama tutasema kuwa inafaa kuitumia kama ushahidi basi ni lazima kubainisha udhaifu wake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (19) http://binothaimeen.net/content/6838
  • Imechapishwa: 14/09/2021