Swali: Ni ipi hukumu kwa yule ambaye hachukui Hadiyth zilizosimuliwa na mpokezi mmoja (حديث الآحاد) katika mambo ya ´Aqiydah?

Jibu: Hukumu yake ni kwamba ni mpotofu na anayepotosha. Ni fikira ya Mu´tazilah. Wanazuoni wamelizungumzia jambo hilo. Imaam ash-Shaafi´iy ameligusia katika “ar-Risaalah”. Imaam al-Bukhaariy ameligusia katika ”al-Musnad as-Swahiyh”. Ibn-ul-Qayyim pia ameandika mada hiyo katika ”as-Swawaa´iq al-Mursalah”. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ

” Kile anachokupeni Mtume, basi kichukueni, na kile anachokukatazeni, basi kiacheni. Mcheni Allaah; hakika Allaah ni mkali wa kuadhibu.”[1]

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ ۖ وَمَن تَوَلَّىٰ فَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا

”Atakayemtii Mtume basi amemtii Allaah, na atakayekengeuka basi hatukukutuma kuwa mlinzi juu yao.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtuma mjumbe mmojammoja.  Bali Allaah (´Azza wa Jall) alimtuma mjumbe mmoja. Wanazuoni walizungumzia suala hili kwa kirefu. Wale wanaoita katika kutupilia mbali masimulizi yaliyosimuliwa na mpokezi mmoja wanaita katika kuibatilisha Shari´ah ya Allaah. Kwa sababu sehemu kubwa ya Hadiyth ni zile zilizosimuliwa na mpokezi mmojammoja. Ni kama tulivosema ni wito wa Mu´tazilah au pengine wa wakanamungu.

[1] 59:07

[2] 04:80

  • Muhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Mu´aanid, uk. 357-358
  • Imechapishwa: 29/06/2025