177 – Muhammad bin Haatim bin Nu´aym ametukhabarisha: Muhammad bin ´Aliy amenikhabarisha: Baba yangu ametukhabarisha: ´Abdullaah ametukhabarisha, kutoka kwa al-Aswad bin Shaybaan, kutoka kwa Khaalid bin Shumayr, kutoka kwa ´Abdullaah bin Rabaah, kutoka kwa Abu Qataadah, ambaye amesimulia:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipanda mimbari na akamwamrisha mwenye kunadi aite: ”Swalah ya mkusanyiko!” Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Khabari mpya zimenifikia! Khabari mpya zimenifikia! Khabari mpya zimenifikia! Je, nisikuelezeni juu ya jeshi lenu linalopambana? Lilisonga mbele mpaka pale ambapo lilikutana na adui. Zayd akauliwa hali ya kuwa ni shahidi. Mwombeeni kwa Allaah msamaha. Kisha Ja´far akashika bendera na kuwashambulia vikali ambapo akauliwa hali ya kuwa ni shahidi. Mimi namshuhudilia kufa shahidi. Mwombeeni msamaha kwa Allaah. Kisha bendera ikachukuliwa na ´Abdullaah bin Rawaahah na akawa imara mpaka alipouliwa hali ya kuwa ni shahidi. Mwombeeni msamaha kwa Allaah. Kisha bendera ikachukuliwa na Khaalid bin al-Waliyd, ambaye hakuwa ni miongoni mwa viongozi.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanyanyua vidole vyake viwili na kusema: ”Ee Allaah, huu ni upanga miongoni mwa panga Zako. Fanya ushindi upatikane kupitia yeye!” Siku hiyo ndio Khaalid aliitwa upanga wa Allaah.”[1]

178 – Ibraahiym bin Ya´quub amenikhabarisha: Wahb bin Zam´ah amenikhabarisha: ´Abdullaah ametukhabarisha, kutoka kwa Sa´iyd bin Yaziyd: Nimemsikia al-Haarith bin Yaziyd al-Hadhwramiy akisimulia kutoka kwa ´Aliy bin Rabaah, kutoka kwa Naashirah bin Sumayy al-Yaziniy, aliyeeleza kuwa amemsikia ´Umar bin al-Khattwaab akiwakhutubia watu:

“Nakuombeni radhi kwa ajili ya Khaalid bin al-Waliyd. Nilimteua kuwapa mali hii wanyonge katika Wahajiri ambapo akawapa wanyonge pamoja na watukufu na wenye ufaswaha. Kwa hiyo nikamtengua na kumteua Abu ´Ubaydah bin al-Jarraah badala yake.” Kisha Abu ´Amr bin Hafsw bin al-Mughiyrah akasema: “Umemtengua mfanyakazi ambaye Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimpa kazi, akachomoa upanga uliochomolewa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akapandisha bendera iliyosimamishwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Umekata udugu na kumhusudu binamu yangu.” Ndipo ´Umar akasema: “Wewe ni jamaa wa karibu, kijana chipukizi na mwenye kukasirika kwa ajili ya binamu yako.”[2]

[1] Ahmad (5/299, 300 na 301). Swahiyh kwa mujibu wa Ahmad Shaakir.

[2] Ahmad (3/475-476). Cheni yake ya wapokezi ni nzuri kwa mujibu wa Ibn Kathiyr katika “Musnad-ul-Faaruuq” (2/478). Wapokezi wake ni wapokezi madhubuti kwa mujibu wa al-Haythamiy katika “Majma´-uz-Zawaa-id” (9/349).

  • Muhusika: Imaam Ahmad bin Shu´ayb an-Nasaa’iy (afk. 303)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaa-il-us-Swahaabah, uk. 118
  • Imechapishwa: 21/09/2026