”Ee Allaah! Kama umeniandika katika watu, Niandike katika wema”

Swali: Nimesoma katika moja ya vitabu vya maelezo ya ”al-Arba´iyn an-Nawawiyyah” maneno yafuatayo:

اللهم إني كتبتني شقيًا فامحني واكتبني سعيدًا

“Ee Mola wangu, iwapo umeniandika miongoni mwa waovu basi nifute na uniandike miongoni mwa wenye kufaulu.”

Ni upi usahihi wa du´aa hii?

Jibu: Du´aa hii imepokelewa kutoka kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa), lakini haina msingi katika Hadiyth Swahiyh. Hakika yule ambaye ameandikwa kuwa ni mwenye maangamizi, atakufa akiwa hivyo, na yule ambaye ameandikwa kuwa ni mwenye kufaulu, atakufa akiwa hivyo. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) humjaalia yule ambaye ameandikwa hali ya kuwa amefaulu kuongozwa katika matendo ya watu wa furaha na kufaulu, na humjaalia yule ambaye ameandikwa hali ya kuwa ni mwovu kuongozwa katika matendo ya watu wa uovu. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ سَعْيَكُمْ لَشَتَّى فَأَمَّا مَن أَعْطَى وَاتَّقَى وَصَدَّقَ بِالْحُسْنَى فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْيُسْرَى وَأَمَّا مَن بَخِلَ وَاسْتَغْنَى  وَكَذَّبَ بِالْحُسْنَى فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْعُسْرَى

“Hakika juhudi zenu bila shaka ni zenye kutofautiana. Basi yule anayetoa na akamcha Allaah na akasadikisha lililo jema zaidi, basi tutamuwepesishia kwa yaliyo mepesi. Ama yule afanyaye ubakhili na akajiona amejitosheleza na akakadhibisha lililo jema zaidi, basi tutamuwepesishia kwa yaliyo magumu.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fanyeni matendo, kwani kila mtu atafanyiwa wepesi kwa kile alichoumbiwa. Watu wa furaha watafanyiwa wepesi kwa matendo ya watu wa furaha, na watu wa maangamizi watafanyiwa wepesi kwa matendo ya watu wa maangamizi.”[2]

[1]92:4-10

[2] al-Bukhaariy (4949) na Muslim (2647).

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/30970/ما-صحة-دعاء-اللهم-اني-كتبتني-شقيا-فامحني
  • Imechapishwa: 22/09/2025