Swali: Ni ipi hukumu ya kumfanyia chanjo mtoto asifikwe na baadhi ya maradhi? Ni ipi hukumu ya kufanya matibabu kwa maradhi ambayo hayajamfika mtu kwa lengo la kujikinga? Ni ipi hukumu ya matibabu ya sumu na dawa zilizo za haramu?

Jibu: Bora ni kujiepusha na chanjo na badala yake mtu akamtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ

“Yeyote anayemtegemea Allaah, basi Yeye humtosheleza.”[1]

Hata hivyo sio haramu kwa sababu sio kwa ajili ya kuondosha maambukizo. Wanachuoni wametofautiana juu ya kuondosha maambukizo; baadhi wamelithibitisha, wengine wamelikanusha na miongoni mwao wamelithibitisha kwa makadirio ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Sahihi ni kwamba hakuna maambukizo kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna maambukizi, kuamini mkosi wa ndege, bundi wala Swafar.”[2]

Chanjo hizi na mfano wake ni kwa lengo la kujikinga. Kama tulivosema hakuna ubaya kufanya hivo na sio haramu wala jambo lililochukizwa. Lakini kwa yule ambaye imani yake ni yenye nguvu na anamtegemea Allaah bora kwake asifanye chanjo:

“Ni wale wasioomba kusomewa matabano, hawajichomi chuma cha moto na wala hawaamini rajua nzuri na mbaya, bali wanamtegemea Mola Wao.”[3]

Kuhusu kujitibisha kwa dawa ambazo ni za haramu, basi itambulike kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Jitibisheni na wala msijitibishe kwa yaliyo ya haramu.”[4]

Vilevile amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah hakufanya shifaa ya Ummah wangu kutokana na yale aliyoharamisha.”

Ikiwa dawa iko na alcohol au kitu kingine kilicho cha haramu, basi haijuzu kujitibu kwacho. Badala yake mtu amtegemee Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Ama kuhusu sumu hali pekee inayojuzu kutumia ni pale ambapo maradhi hayawezi kuondoka isipokuwa kwa kuitumia na sambamba na hilo sumu hiyo haiathiri ini wala viungo vyengine. Uhakika wa mambo ni kwamba sumu inaingia ndani ya zile dawa zilizoharamishwa. Ikiwa sumu inapelekea kuleta maradhi mengine basi itakuwa ni lazima kuiepuka. Hili ni mosi.

Jambo jengine ni kwamba kile kilicho haramu kinaweza kugeuzwa na kikatokomea. Kwa mfano najisi ambazo zimechomewa moto mpaka mwishowe zikawa majivu. Hivyo majivu hayo yanapoteza uharamu wake. Mfano mwingine ni pombe ambayo inageuka kuwa siki. Baadhi ya wanachuoni wameita juu ya maafikiano ya unajisi wa pombe. Vile ninavoona ni kwamba pombe sio najisi; ni haramu lakini hata hivyo sio najisi. Si kila ambacho ni haramu kinakuwa najisi.

Swali: Chanjo zinakuwa na sumu lakini zinatolewa kwa lengo la kuzuia maradhi.

Jibu: Ikiwa sumu hii haidhuru basi – Allaah akitaka – haina neno. Inachukuliwa kwa lengo la kuzuia maradhi na sio kwa ajili ya kuondosha maambukizo.

[1] 65:03

[2] al-Bukhaariy (5757) na Muslim (2220).

[3] al-Bukhaariy (5705) na Muslim (2220).

[4] Abu Daawuud (3874).

  • Mhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.muqbel.net/fatwa.php?fatwa_id=675
  • Imechapishwa: 03/12/2020