Baba anakataa kumuozesha msichana wake kwa mposaji aliye na kazi duni

Swali: Unasemaje kuhusu mtu ambaye hamuozi binti yake kwa mpiga chuku, mchinjaji au fundi chuma hata ikiwa huyo mwanaume ni mtu wa dini na mwenye tabia njema? Je, tendo hili ni sahihi kwa kudhani kwamba kazi ya kuchinja au kupiga chuku ni aibu katika ndoa?

Jibu: Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا ۚ إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ

“Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamme na mwanamke na tukakufanyeni kuwa mataifa na makabila ili mtambuane. Hakika aliye mbora zaidi miongoni mwenu mbele ya Allaah ni yule mwenye kumcha Allaah zaidi kati yenu. Hakika Allaah ni Mjuzi, Mwenye khabari za ndani na za nje.”[1]

Kwa hiyo ikipatikana mwenye kumcha Allaah zaidi ndiye aozeshwe, ni mamoja awe ni mwarabu au asiye mwarabu, kutoka katika kabila la kizazi cha Haashim au wengineo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaambia Answaar:

”Enyi wana wa Bayaadhwah! Oeni kwa Abu Hind na muozeshe kwake.”

Alikuwa ni mtu mwenye kupiga chuku.

Makusudio ni kwamba kipimo ni matendo mema na kumcha Allaah. Kazi yake ya kuumika, fundi chuma, mshona viatu au seremala haidhuru. Daawuud (´alayhis-Salaam) alikuwa fundi chuma akitengeneza ngao na kuziuza na yeye ni Nabii wa Allaah. Kwa hiyo ni wajibu kwa muumini kumtafutia msichana wake mwenye kumcha Allaah. Akiwa anatokana na nasaba njema pia, ni kheri juu ya kheri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mwanamke huolewa kwa mambo manne; mali yake, nasaba yake, uzuri wake na dini yake. Mchague yule mwenye dini mkono wako upige mchanga.”

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Mtu akikuja kuomba uchumba kwenu ambaye mnaridhika na dini yake na tabia yake, basi muozesheni.”

Hajasema nasaba yake, bali amesema:

”… ambaye mnaridhika na dini yake na tabia yake, basi muozesheni. Msipofanya hivyo itakuwa fitina ardhini na ufisadi mkubwa.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwozesha Faatwimah bint Qays kwa Usaamah bin Zayd, mtumwa aliyeachwa huru, mtoto wa mtumwa aliyeachwa huru. Faatwimah bint Qays alikuwa ni kutoka katika kabila la Quraysh. Abu Hudhayfah bin ´Utbah alimwozesha Saalim, mtumwa wake aliyemwacha huru, msichana wake.

Makusudio ni kuwa muumini anatafuta kazi njema na uchaji Allaah, pasi na kujali ametoka wapi au anafanya kazi gani, mradi awe na dini na tabia njema. Kama Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyosema:

”Mtu akikuja kuomba uchumba kwenu ambaye mnaridhika na dini yake na tabia yake, basi muozesheni.”

[1] 49:13

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/31025/حكم-من-لا-يزوج-ابنته-لحجام-او-جزار-او-حداد
  • Imechapishwa: 29/09/2025