Baadhi ya mifano ya Sunnah na mambo ya kawaida

Swali: Tunatambuaje tofauti kati ya kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa ni Sunnah au ni jambo la kawaida?

Jibu: Msingi ni kwamba vitendo vyake ni Sunnah. Hilo ndilo msingi:

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ

“Hakika mna kigezo kizuri kwa Mtume wa Allaah.”[1]

Isipokuwa pale panapojulikana kupitia dalili nyingine kwamba kitendo hicho ni katika mambo ya kawaida ambayo Mtume hakikuamrisha chochote juu yake, wala hakudumu kukifanya. Mfano wake ni aina za vyakula, aina za mavazi na mambo yaliyofanana nayo ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwa akiyafanya kwa kudumu. Hayo yanaonyesha kuwa ni mambo ya kawaida. Mfano mwingine ni suala la kutunza nywele za kichwani au kuzinyonyoa, pia kuvaa kanzu au kikoi na nguo ya juu.

Swali: Kuna msemo unaosema kuwa kitendo ambacho hakina thawabu maalum, kukatazwa, wala kuamrishwa, basi kinakuwa ni ada tu.

Jibu: Msingi ni kumuiga Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mambo yote, isipokuwa yale yaliyothibiti kwa dalili kuwa ni mambo ya kawaida ambayo hakuwa akiyafanya kwa kudumu. Hayo yanabaki kuwa ya kawaida; wakati mwingine akiyafanya na wakati mwingine kuyaacha, kama aina za mavazi na aina za vyakula na mfano wake.

Swali: Je, mtu kama akifuata mambo haya ya kawaida anapata thawabu?

Jibu: Allaah ndiye anajua zaidi.

[1] 33:21

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/31630/ما-كيفية-تمييز-السنة-او-العادة-من-فعل-النبي
  • Imechapishwa: 21/12/2025