Baadhi ya Aayah na Hadiyth zinazokemea Bid´ah na uzushi

05- Mama wa waumini Umm ´Abdillaah ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza kuwa “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuzusha katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo, basi atarudishiwa mwenyewe.”

Makusudio ya Hadiyth hii ni Bid´ah katika dini. Bid´ah katika dini Hadiyth zimeonesha kuwa inarudishwa. Kuna Aayah na Hadiyth nyingi zimeonyesha hivo. Allaah (Ta´ala) Amesema:

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ

“Je, wanao washirika waliowaamuru dini yale ambayo Allaah hakuyatolea kwayo idhini?” (42:21)

Amewaita kuwa ni washirika kwa kuwa wameweka katika Dini kitu ambacho hakikuleta Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Allaah Hakukiidhinisha katika Shari´ah. Allaah (Ta´ala) Amesema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

“Leo Nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.” (05:02)

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ

“Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni Atakupendeni Allaah.” (03:31)

Aayah zilizo na maana kama hii ni nyingi ikiwa ni pamoja na Kauli Yake (Jalla wa ´Alaa):

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

“Na lolote lile analokupeni Mtume basi lichukueni na analokukatazeni, basi acheni.” (59:07)

Imethibiti katika Hadiyth Bid´ah na uzushi kulaumiwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema katika Khutbah ya Ijumaa na kwenginepo:

“Kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni.”

Vilevile imethibiti katika Sunan Hadiyth ya al-´Irbaadhw bin Saariyah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Siku moja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitupa mawaidha yaliyozitikisa nyoyo zetu na yakatutoa machozi. Tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Kana kwamba ni mawaidha ya kuaga, basi tuusie.”

Miongoni mwa mambo aliyousia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni pamoja na:

“Hakika yule atakayeishi katika nyinyi basi ataona tofauti nyingi. Hivyo basi, jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu. Ziumeni kwa magego. Tahadharini na mambo ya kuzua. Hakika kila kitachozushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Arba´iyn an-Nawawiyyah, uk. 124-125
  • Imechapishwa: 17/05/2020