Swali:

بسم الله الرحمن الرحيم

السلام عليكم و رحمة الله و بركاته

Ndugu jamaa zake na maiti wafanye nini baada ya kumzika maiti? Je, wakae nyumbani kwa muda wa siku tatu na wasome Qur-aan juu ya roho ya maiti? Je, mtu amlete nyumbani msomaji Qur-aan na amlipe kwa kile kisomo chake? Akubali tanzia pale mazishini peke yake au akae nyumbani na kupokea tanzia pasi na kuwepo msomaji Qur-aan? Je, thawabu za kisomo hiki kinamfikia maiti? Ni ipi njia sahihi ya kufanya kwa wale ndugu jamaa wa maiti baada ya msiba?

Jibu:

بسم الله الرحمن الرحيم

و عليكم السلام و رحمة الله و بركاته

Kuketi nyumbani kwa ajili ya kupokea tanzia ni Bid´ah na mambo mepya. Kitu kama hicho hakikuwepo katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala wakati wa Maswahabah zake waongofu. Bali Jariyr bin ´Abdillaah al-Bajaliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Walikuwa wakizingatia kukusanyika kwa familia ya maiti na kutengeneza chakula baada ya mazishi ni aina fulani ya kuomboleza.”[1]

Baya zaidi kuliko hayo ni kukodisha msoma Qur-aan aje kusoma Qur-aan kwa ajili ya roho ya maiti. Usomaji Qur-aan ni ´ibaadah na si jambo kimewekwa katika Shari´ah kwa mnasaba huu. Isitoshe haisihi kuchukua malipo kwa ajili ya ´ibaadah. Yule msoma Qur-aan aliyekodishwa halipwi mbele ya Allaah, kwa sababu ameharakisha malipo yake hapa duniani. Kwa ajili hiyo maiti yule hanufaiki kwa kisomo chake cha Qur-aan.

Baada ya maziko mtu anatakiwa kusimama karibu na kaburi na kumuombea kwa Allaah msamaha na uimara. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwombeeni msamaha ndugu yenu na mtakieni uimara; kwani hakika hivi sasa anahojiwa.”[2]

Kwa hivyo mtu asimame karibu na kaburi na aseme:

اللهم اغفر له، اللهم اغفر له، اللهم اغفر له. اللهم ثبته، اللهم ثبته، اللهم ثبته

“Ee Allaah! Msamehe! Ee Allaah! Msamehe! Ee Allaah! Msamehe! Ee Allaah! Mthibitishe! Ee Allaah! Mthibitishe! Ee Allaah! Mthibitishe!”

Kisha baada ya hapo aondoke zake.

Kuhusu tanzia, ni sawa kuwapa pole wale ndugu jamaa zake maiti. Mtu anatakiwa kuwaambia:

اصبر و احتسب، فإن لله ما أخذ، و له ما أبقى، و كل شيء عنده بأجل مسمى

“Subirini na tarajieni malipo kutoka kwa Allaah. Ni Chake Allaah alichokitwaa na Yeye Chake alichokibakiza na kila kitu Kwake kina muda maalum.”

Hakuna haja ya kukusanyika, kuwasha mataa, kutenga viti na kumleta msomaji Qur-aan, yote haya ni katika Bid´ah na mambo yaliyozuliwa. Tunamuomba Allaah atupe sisi na ndugu zetu uimara juu ya Sunnah na uokozi kutokamana na Bid´ah. Kwani hakika Yeye ni mwenye kusikia na mwenye kuitikia.

Muhammad bin Swaalih al-´Uthaymiyn

1410-10-19

[1] Ahmad (2/204) na Ibn Maajah (1612). ash-Shawkaaniy amesema:

”Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.” (Nayl-ul-Awtwaar)

[2] Abu Daawuud (3221).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/395-396)
  • Imechapishwa: 09/06/2021