Asili (nature) haiwezi kufanya chochote

Swali: Mtu alimwambia rafiki yake: “Je, umesikia khabari za matetemeko ya ardhi yaliyosababishwa na asili katika nchi fulani?” Rafiki yake akajibu: “Asili haina akili?”

Jibu: Ndiyo, hili ni kosa. Maneno yake: “asili imefanya” au “asili imesababisha” ni kosa. Asili si kitu kinachofanya. Asili ni sifa miongoni mwa sifa za vitu. Kila kitu kina asili yake: maji yana asili yake, moto una asili yake na binadamu ana asili yake. Hivyo asili ni sifa iliyosimama kwa kitu kingine. Haina uwezo wa kufanya yenyewe. Lakini haya ni katika ujinga wa wajinga na kufuata kipofu. Huyu ni mjinga na huyu ni mfuataji kichwa mchunga. Hakuna kitu kinachoitwa asili kinachofanya chochote. Bali ni sifa zilizopo katika vile vinavyoelezewa. Asili ya moto ni kuunguza, asili ya maji ni kuwa maji (mtiririko), asili ya binadamu ni hivi na asili ya mnyama mwingine ni vile. Hivyo kila kitu kina asili yake maalum ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amekiweka juu yake na amekiumba juu yake. Muumba ni Allaah peke yake, Yeye ndiye Muumba, Mjuzi (Subhaanahu wa Ta´ala):

أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ

“Tanabahi! Uumbaji ni Wake pekee na kupitisha amri.”[1]

اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ

”Allaah ni Muumbaji wa kila jambo.”[2]

Hakuna chochote kinachoumba isipokuwa Allaah, si asili wala kitu kingine. Basi asili ni sifa iliyosimama kwa kile chenye asili hiyo. Haya yameenea katika ndimi za watu wengi wa batili miongoni mwa wapinga dini na wengine miongoni mwa wajinga wanawaiga.

[1] 07:54

[2] 39:62

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3413/حكم-قول-هذا-شيء-فعلته-او-احدثته-الطبيعة
  • Imechapishwa: 09/09/2026