Swali: Ni ipi hukumu ya mtu ambaye anaswali baadhi ya nyakati? Je, inafaa kutaamiliana naye na kufanya naye urafiki?

Jibu: Ikiwa kunakusudiwa kuacha swalah ya mkusanyiko, basi kitendo chake ni haramu na kinamfanya kuwa fasiki. Kwa sababu ni wajibu kuswali swalah ya mkusanyiko msikitini na wala mtu asiiiache isipokuwa kutokana na udhuru unaokubalika katika Shari´ah.

Ikiwa haswali kabisa na anafanya hivo kwa imani, basi hilo linamfanya kuwa kafiri na kunamtoa katika Uislamu. Anayepinga uwajibu wa swalah ni kafiri isipokuwa ikiwa kama ndio punde ameingia katika Uislamu na hajui juu ya faradhi na mambo ya Shari´ah ya Uislamu. Katika hali hiyo anatakiwa kubainishiwa haki. Akiendelea kung´ang´ania kuipinga basi anakuwa kafiri na mwenye kuritadi.

Lakini ikiwa anakubali kuwa swalah ni wajibu lakini hata hivyo nafsi yake inamshinda kutokana na uvivu na uzembe, basi wanazuoni wametofautiana juu ya ukafiri wake. Wako ambao wanaona kuwa mwenye kuacha swalah ya faradhi mpaka ukatoka wakati wake, basi anakuwa kafiri. Wako wengine ambao wanaona kuwa hawi kafiri mpaka pale atakapoiacha kabisa. Haya ndio maoni sahihi; ni lazima aiache kabisa ili awe kafiri, kwa sababu atakuwa si mwenye kujali swalah. Kwa ajili hiyo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Baina ya mtu na kufuru na shirki ni kuacha swalah.”[1]

Udhahiri wa Hadiyth ni kuiacha kabisa. Vivyo hivyo Hadiyth ya Buraydah:

“Ahadi iliopo kati yetu sisi na wao ni swalah. Hivyo basi, yule atakayeiacha amekufuru.”[2]

Hakusema “yule mwenye kuacha swalah”. Kwa hali yoyote ni kwamba mimi naona kuwa hakufuru isipokuwa mpaka pale atakapoiacha kabisa.

Kuhusiana na swali, naona kuwa hakufuru. Hata  hivyo anazingatiwa kuwa ni fasiki na anatokwa na sifa ya uadilifu; kwa ajili hiyo hana haki ya kuwa na usimamizi juu ya ndugu zake, haukubaliwi ushahidi wake na wala hawezi kuwa kiongozi juu ya waislamu.

Kuhusiana na kutangamana na kufanya naye urafiki, hapana vibaya ikiwa kunatarajiwa juu yake kutengemaa. Vinginevyo hapana. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mfano wa matangamano mabaya ni kama mhunzi. Ima akakuchomea nguo yako ukapata harufu ya uvundo wake.”[3]

[1] Muslim (82).

[2] at-Tirmidhiy (2621), an-Nasaa’iy (463) na Ibn Maajah (1079). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

[3] al-Bukhaariy.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/51-52)
  • Imechapishwa: 14/07/2026