Anasema kuwa yuko huru baada ya kukemewa maovu

Swali: Baadhi ya watu ukiwaamrisha na kuwakataza husema mmoja wao kwamba yeye yuko niko huru na huna haki ya kuingilia wala wala huingii nami kaburini. Tunaomba ufafanuzi wa hilo na mipaka ya uhuru unaoruhusiwa kwa mujibu wa maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ

“Hapana kulazimisha katika dini.”[1]

Kadhalika baadhi ya watu ukiwaamrisha au kuwakataza maovu, kama baadhi ya vyombo vya khabari na mfano wake, husema kwamba lau kama kuna ubaya, basi serikali isingelileta na mengineyo?

Jibu: Hii ni kosa. Kusema kwake kwamba yeye yuko huru ni kosa, hili ni neno la kishaytwaan halifai. Hayuko huru katika kuacha yale aliyoyalazimisha Allaah au kufanya yale aliyoyaharamisha Allaah. Yeye ni huru katika kutumia mali yake na kufanya biashara ikiwa ni mwenye akili timamu. Yeye ni huru katika mambo hayo. Lakini katika kufanya maasi ya Allaah au kuacha yale aliyoyalazimisha Allaah, si huru. Bali ni lazima ajifunge na dini, ashikamane na dini na asipingane na yale aliyoyatunga Allaah. Ndugu zake wanawajibika kumkemea akivuka mipaka, akaacha wajibu au baadhi ya wajibu au akafanya baadhi ya yaliyoharamishwa si huru. Bali ni lazima akemewe na ni lazima ajifunge na Shari´ah ya Allaah. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

تِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ فَلَا تَعْتَدُوهَا

”Hiyo ni mipaka ya Allaah, hivyo basi msiivuke.”[2]

Amesema kuhusu maasi:

تِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ فَلَا تَقْرَبُوهَا

”Hiyo ni mipaka ya Allaah, hivyo basi msiikaribie.”[3]

Kwa hiyo muumini amepewa amri, muislamu amepewa amri ashikamane na mipaka, asivuke mipaka, ajifunge na Shari´ah ya Allaah na ajiepushe na yaliyoharamishwa na Allaah.

Kusema kwamba ”Mimi niko huru, hutokuwa nami kaburini”, hii ni kosa. Maneno haya ni katika hila za shaytwaan. Shaytwaan anapenda kila mmoja aseme hivi ili asikubali kutoka kwa ndugu yake.

Vilevile kusema kwamba lau hili lingekuwa ni ovu basi lisingeingia nchini au serikali isingeliruhusu, hili ni kosa. Serikali haikukingwa na makosa. Inaweza kutokea kwake yanayotokea kwa wengine katika makosa na kupotoka. Huenda kitu kikaingia kwa siri bila kujua na huenda kikapatikana kati ya watu kile ambacho serikali haikukiruhusu.

Ninachotaka kusema ni kwamba serikali si kipimo. Kipimo ni yale aliyosema Allaah na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Serikali inaweza kukosea, inaweza kufanya makosa na inaweza kuasi. Haikukingwa na makosa. Serikali si hoja katika kuhalalisha yale aliyoyaharamisha Allaah wala katika kuacha yale aliyoyalazimisha Allaah. Haya hayasemi isipokuwa mjinga asiyejua Shari´ah. Shari´ah ni yale aliyosema Allaah na Mtume Wake, si yale yaliyosemwa na serikali fulani na fulani.

[1] 02:256

[2] 02:229

[3] 02:187

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3368/حكم-من-امر-بمعروف-فقال-انا-حر
  • Imechapishwa: 20/09/2026