Ana wasiwasi sana katika twahara na swalah yake kutokana na gesi nyingi tumboni

Swali: Mtu anakuwa na hewa nyingi tumboni, pengine gesi, kiasi kwamba anapata shida kukamilisha wudhuu´. Kwa mfano anapofika kwenye kuosha uso huhisi hisia nyepesi na kuingiwa na khofu kwamba huenda wudhuu´ wake umeharibika. Matokeo yake huanza wudhuu´ upya. Vivyo hivyo wakati wa kuswali huhisi hali kama hiyo bila kunusa harufu yoyote. Suluhisho la jambo hili ni lipi?

Jibu: Wasiwasi huu unatoka kwa shaytwaan ambaye anataka kuharibu ´ibaadah ya muislamu. Kwa hiyo ni wajibu kuupuuza na muislamu asitoke katika swalah yake wala kurudia wudhuu´ wake isipokuwa pale anaposikia sauti au kuhisi harufu. Imepokelewa na Imaam Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mmoja wenu anapohisi kitu tumboni mwake, kisha akawa na shaka kwamba, je, kimetoka kwake kitu au hakikutoka, basi asiondoke msikitini mpaka asikie sauti au ahisi harufu.”[1]

Kinachokusudiwa ni mtu kuwa na uhakika kwamba hadathi imetoka. Maadamu bado ana shaka hata kidogo, basi twahara yake ni sahihi.

[1] Muslim (01/190).

  • Muhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (5/226-227)
  • Imechapishwa: 09/11/2026