Adhkaar za kuwafukuza majini na mashaytwaan ambazo hazikuthibiti

Swali: Nimesoma katika kitabu ”Wiqaayat-ul-Insaan minal-Jinn wash-Shaytwaan” chini ya kichwa cha khabari kinachosema ”Kayfa Tatwrud-ul-Jinn minal-Bayt”. Mtunzi akasema:

”Ikiwa utayakini kabisa kwamba nyumba yumo jini, basi njia ya kumtoa ni kama ifuatavyo: unaenda wewe na wenzako wawili katika nyumba hiyo na kusema: ”Nawashinikiza kwa ahadi aliyowachukulia Sulaymaan mtoke au mhame kutoka nyumba yetu. Nawashinikiza kwa Allaah mtoke wala msimdhuru yeyote na kwamba urudie kusema hvio siku tatu. Ukihisi baada ya hapo bado kuna kitu ndani ya nyumba, basi ulete maji katika chombo, uweke kidole chako ndani yake na kukikaribia kinywa chako na kusema: ”Kwa jina la Allaah tumemwamini Allaah ambaye hakuna kitu kinachojikinga kutokana Naye, kwa utukufu wa Allaah usioweza kudhalilishwa na kwa mamlaka ya Allaah yenye nguvu tunajikinga… ” Kisha usome Suurah ”as-Swaaffaat” mpaka katika maneno Yake (Ta´ala):

فَأَتْبَعَهُ شِهَابٌ ثَاقِبٌ

”… kitamwandama kimondo kiwakacho.”[1]

Kisha baada ya hapo uyazungushe maji katika pembe za nyumba, basi watatoka humo kwa idhini ya Allaah (Ta´ala). Je, ipi hukumu ya kufanya hivo?

Jibu: Hayana dalili. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameelekeza lililo fupi zaidi ya hili.  Amesema mtu aseme:

أَعُوْذُ بِكَلِماتِ اللَّهِ التَّامَّتِ مِنْ شَرِّ مَا خَلَقَ

”Najilinda kwa maneno ya Allaah yaliyotimia kutokamana na shari Alivyoviumba.”[2]

Hivi ndivyo alivyosema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Yeyote mwenye kushuka mahali akasema:

أَعُوْذُ بِكَلِماتِ اللَّهِ التَّامَّتِ مِنْ شَرِّ مَا خَلَقَ

”Najilinda kwa maneno ya Allaah yaliyotimia kutokamana na shari Alivyoviumba.”,

hakitomdhuru kitu chochote mpaka aondoke mahali pake hapo. Basi akihisi kitu, aseme haya na arudie:

أَعُوْذُ بِكَلِماتِ اللَّهِ التَّامَّتِ مِنْ شَرِّ مَا خَلَقَ

”Najilinda kwa maneno ya Allaah yaliyotimia kutokamana na shari Alivyoviumba.”,

Vivyo hivyo aseme:

بسم الله الذي لا يضرُّ مع اسمه شيءٌ في الأرض ولا في السماء، وهو السميع العليم

“Kwa jina la Allaah ambaye hakidhuru kwa jina Lake chochote mbinguni na ardhini Naye ni Mwenye kusikia, Mjuzi wa yote.”

Vilevile azidishe kusoma Qur-aan. Inatosha kufanya hivo. Haya ndiyo aliyoyaelekeza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akawafundisha ummah wake. Ikiwa kimejaribiwa kitu cha chumvi ikanyunyizwa nyumbani au kitu kingine kikasaidia, basi hapana vibaya. Ikiwa kimejaribiwa kitu kikawadhuru na kuwatoa miongoni mwa vile vitu vilivyoruhusiwa, hapana vibaya. Lakini msingi ni yale aliyoyabainisha na kuyaelekeza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 37:10

[2] Ahmad (02/290), an-Nasaa´iy katika “‘Amal-ul-Yawm wal-Laylah” (590) na Ibn-us-Sunniy (68). Tazama “Swahiyh-ut-Tirmidhiy (03/187), “Swahiyh Ibn Maajah” (92/266), “Tuhfat-ul-Akhyaar”, uk. 45.)

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/30930/حكم-بعض-الادعية-التي-تقال-لطرد-الشيطان
  • Imechapishwa: 14/09/2025