Adhaana ya Fajr ni 1 au 2?

Swali: Fajr ina adhaana mbili. Je, hili ni Sunnah ya lazima au ni jambo linalopendeza tu? Je, hilo hufanyika katika Ramadhaan tu au katika miezi yote ya mwaka? Muda wake ukoje?

Jibu: Adhaana ya wajibu ni moja tu. Adhaana ya pili inapendeza endapo kutakuwa na haja ya kufanya hivyo. Hakuhifadhiwa kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliifanya isipokuwa katika Ramadhaan. Bilaal (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa akitoa adhaana ya kwanza ili kuwaamsha waliolala na kumtanabahisha anayeswali usiku, muda mfupi kabla ya Fajr. Haikuhifadhiwa kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kipindi kisicho Ramadhaan.

Hata hivyo baadhi ya wanazuoni wamelipendelea jambo hili kwa ujumla kwa ajili ya kutoa tanbihi, kwa kuwa inawatanabahisha watu juu ya kukaribia kuchomoza kwa Fajr ili watu wajitayarishe na mwenye kufunga ajue wakati unakaribia. Lakini suala hili ni lenye wasaa. Adhaana ya lazima ni ile ya Fajr tu. Lakini ya kwanza si ya wajibu, bali ni jambo linalopendekezwa tu endapo kunakuwa na haja.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1108/هل-النداء-باذانين-في-صلاة-الفجر-مشروع
  • Imechapishwa: 25/01/2026