95. Kitenguzi cha sita: Mwenye kufanya istihzai na mambo ya dini

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

La sita:

Mwenye kufanyia istihzai kitu katika dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), thawabu yake  au adhabu yake, basi amekufuru. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَلَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?” Hivyo msitoe udhuru, kwani mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.(at-Tawbah 09 : 65-66)

MAELEZO

Maneno Yake:

La sita… – Miongoni mwa vichenguzi vya Uislamu.

Mwenye kufanyia istihzai… – Huu ni mlango mkubwa.  Ulio kabla yake ni kuhusu mwenye kuchukia kitu katika aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuchukia ni katika matendo ya kimoyo. Ama kufanya istihzai ni katika kauli za ulimi.

Aayah hii tukufu sababu ya kuteremka kwake ni kwamba kulikuwepo kundi katika waislamu walikuwa wanapigana Jihaad bega kwa bega pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika vita vya Tabuuk. Wakakusanyika katika majlisi ambapo mmoja wao akasema:

“Hatujapata kuona watu kama wasomaji wetu hawa, matumbo yao yanapenda kula sana, ndimi zao zinasema uongo sana na ni waoga wakati wa mapambano.”

Wanamkusudia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum).

Katika majlisi hiyo kulikuwa kijana kutoka katika Answaar, aitwaye ´Awf bin Maalik, ambaye alimwambia mtu huyu:

“Hakika umesema uongo, isipokuwa wewe tu ni mnafiki. Nitamwambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” ´Awf akasimama na kwenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumweleza aliyoyasema ambapo akakuta Wahy imekwishamtangulia na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekwishateremshiwa. Allaah akamweleza waliyosema watu hawa katika majlisi haya au mambo hayo yalisemwa na mmoja katika wao ambapo wengine hawakumkemea. Pindi maneno haya mabaya yalipomfikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatoka mahali alipokuwa amekaa na akapanda kipando chake. Akaja mtu huyu, aliyeongea maneno yale, kutoa udhuru na huku akisema:

“Ee Mtume wa Allaah! Hakika sisi tulikuwa tunafanya porojo na tunacheza. Tulikuwa tukiongea tu ili kufupisha urefu wa safari. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hamtazami na huku ameshikilia kamba za ngamia wake. Mtume hamtazami na hakuna anachozidisha zaidi ya kusoma Aayah ifuatayo:

أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَلَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?” Hivyo msitoe udhuru, kwani mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.” (at-Tawbah 09:65-66)

Maneno Yake (Jalla wa ´Alaa):

قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“… kwani mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.”

ni dalili inayoonyesha kwamba walikuwa waumini na hawakuwa wanafiki. Ni dalili vilevile inayoonyesha kwamba yule mwenye kufanya istihzai na Allaah, Mtume Wake au  kitu kilichokuja kutoka kwa Allaah na Mtume Wake, anakufuru baada ya kuamini kwake na anaritadi kutoka katika Uislamu. Hii ndio nukta muhimu katika Aayah. Lau kama wangelikuwa ni wanafiki basi Asingelisema:

قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“… kwani mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.”

Kwa sababu kimsingi wanafiki sio waumini. Hawaitwi ´waumini`. Isipokuwa wanaitwa ´wanafiki`. Katika Aayah nyingine Allaah amesema kuhusu wanafiki:

وَلَقَدْ قَالُوا كَلِمَةَ الْكُفْرِ وَكَفَرُوا بَعْدَ إِسْلَامِهِمْ

”… na hali wamekwishasema neno la kufuru na wakakufuru baada ya Uislamu wao.” (at-Tawbah 09:74)

Hakusema:

“… baada ya kuamini kwao.”

Uislamu maana yake ni kule mtu kutangaza kuingia katika Uislamu, japokuwa atakuwa si mkweli ndani ya moyo wake, bali huenda ndani ya moyo wake akawa ni kafiri hata kama kwa uinje akaonyesha Uislamu. Huyu ndiye mnafiki. Aayah hii haikusema kuwa wamekufuru baada ya kuamini kwao, bali imesema

وَكَفَرُوا بَعْدَ إِسْلَامِهِمْ

“… wakakufuru baada ya Uislamu wao.”

Kuna tofauti  kati ya Uislamu na imani.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 127-130
  • Imechapishwa: 17/12/2018