Kusema kwamba imani inazidi kwa utiifu ni jambo limetajwa ndani ya Qur-aan. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَيَزِيدُ اللَّهُ الَّذِينَ اهْتَدَوْا هُدًى

“Awazidishie Allaah wale waliooongoka uongofu.”[1]

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ

“Hakika si venginevyo waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah, basi nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayah Zake huwazidishia imani na kwa Mola wao wanategemea.”[2]

وَإِذَا مَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ فَمِنْهُم مَّن يَقُولُ أَيُّكُمْ زَادَتْهُ هَـٰذِهِ إِيمَانًا ۚ فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا فَزَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَهُمْ يَسْتَبْشِرُونَ

“Na inapoteremshwa Suurah, basi miongoni mwao wako wanaosema: “Nani kati yenu [Suurah] hii imemzidishia imani?” Ama wale walioamini huwazidishia imani nao wanafurahia.”[3]

Aayah zinafahamisha kwamba imani inazidi. Kadhalika imani inapungua kwa maasi na upungufu wa matendo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“… ya chini yake ni kuondosha chenye kuudhi njiani.”[4]

Vilevile amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule miongoni mwenu atakayeona maovu basi ayazuie kwa mkono wake. Asipoweza, basi afanye hivo kwa mdomo wake. Asipoweza, basi afanye hivo kwa moyo wake na hiyo ni imani dhaifu mno.”[5]

Katika tamko lingine imekuja:

“… nyuma ya hilo hakuna imani sawa na kiasi cha mbegu ya hardali.”[6]

Ni dalili inayojulisha kuwa imani inaweza kuwa dhaifu, inaweza kuwa ndogo na inaweza kuwa sawa na mbegu ya hardali. Katika Hadiyth nyingine Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) anasema:

“Mtoeni Motoni yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na dinari, kisha yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na nusu dinari, kisha yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na kokwa ya tende, kisha yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na dudu mchungu na halafu yule ambaye yuko na imani ya chini chini chini kabisa kuliko dudu mchugu.” [7]

Allaah atamwokoa muumini kutokamana na Moto kutokana na imani yake ndogo sawa na mbegu ya hardali. Ni dalili inayojulisha kuwa imani inazidi na kupungua. Inazidi kwa matendo mema na inapungua kwa maasi. Kila ambavo utamtii Allaah kwa wingi basi imani yako ndivo inazidi. Kila ambavo utamuasi Allaah kwa wingi basi imani yako ndivo inapungua. Kuongezeka na kupungua kwa imani kunategemea matendo. Matendo mema yakiwa mengi basi imani inazidi. Matendo mema yakiwa machache basi imani inapungua.

[1] 19:76

[2] 8:2-4

[3] 09:124

[4] al-Bukhaariy (9) na Muslim (35).

[5] Ahmad (3/10) na Muslim (49).

[6] Muslim (50).

[7] al-Bukhaariy (7510) na Muslim (193).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 72-73
  • Imechapishwa: 25/08/2021