94. Udhahiri kana kwamba ni udhalili kwa waislamu lakini mwishowe ikawa utukufu na ushindi

Kwa haya tunapata kubainikiwa kwamba ni wajibu kwa muislamu kupokea na kuiheshimu Qur-aan cha Allaah (´Azza wa Jall) na Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na asivitangulizie chochote katika maoni, madhehebu, matakwa na matamanio mbalimbali. Haya ndio yanayopelekewa na imani. Vilevile anatakiwa kuipenda Qur-aan na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na achukie vinavyokwenda kinyume na Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hii ndio alama ya imani, ufuataji na uigaji. Allaah (Ta´ala) ameteremsha Qur-aan na Sunnah na akatuamrisha kufuata Qur-aan na Sunnah. Sambamba na hayo ametukataza kwenda kinyume navyo. Yule ambaye anataka kuokoka na anataka Pepo basi ni lazima kwake kushikamana barabara na Qur-aan na Sunnah japokuwa vitakwenda kinyume na yale anayoyataka na anayoyatamani. Mwisho ni wenye kusifiwa. Allaah (Jalla wa ´Ala) ni Mwingi wa hekima na mjuzi wa yote. Yeye ndiye kakuharamishia kitu hichi hata kama unakipenda kitu hichi. Lakini Allaah ndiye anajua mwisho wake. Amesema (Ta´ala):

كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِتَالُ وَهُوَ كُرْهٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ

”Mmeandikiwa kupigana vita nako ni chukizo kwenu na huenda mkachukia jambo na hali lenyewe ni kheri kwenu na huenda mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu; na Allaah anajua na nyinyi hamjui.” (al-Baqarah 02:216)

Wanachukia vita kutokana na ule ugumu, majeraha, mauaji na ukhatari unaopatikana ndani yake. Ni machukizo ya kimoyo na sio machukizo ya kidini. Kwa sababu moyo unachukia majeraha na mauaji:

وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ

“Huenda mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu; na Allaah anajua na nyinyi hamjui.”

Muislamu anapaswa kutambua ya kwamba yale Allaah aliyohukumu au Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi ndio yenye kheri hapa duniani na huko Aakhirah. Mambo ni hivo japokuwa itaionekana kwake kuwa yana ugumu na yanakwenda kinyume na matamanio ya nafsi. Anatakiwa kuamini kwamba kheri ni kwa yale aliyosema Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Asiyatangulizie mawili hayo chochote na wala asiyatangulizie maoni yake. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيِ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

”Enyi mlioamini! Msitangulize mbele ya Allaah na Mtume Wake. Mcheni Allaah! Hakika Allaah ni Mwenye kusikia, mjuzi wa yote.” (al-Hujuraat 49:01)

´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Enyi watu! Zituhumuni rai zenu juu ya dini. Lau ungeniona siku ya Abu Jandal nilivyokuwa nataka kurudisha amri ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo nikajitahidi na sikupatia.”[1]

Kisa chenyewe ni pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipotaka kufunga mkataba na washirikina katika Hudaybiyah ambapo wakapatana arudi nyuma na aje tena mwaka ujao. Hilo likawa gumu kwa ´Umar na Maswahabah wengine. Kwa sababu ilionekana ni kama kwamba ni kuwapa ushindi makafiri na ndani yake kuna udhalilifu kwa waislamu. Ndipo wakayaona magumu ambapo ´Umar akazungumza na Abu Bakr. Lakini Abu Bakr akamjibu:

“Huyu ni Mtume wa Allaah. Shikamana na kamba yake.”

Mambo yakamalizika vizuri na ikawa ni kheri kwa waslamu na utwevu kwa makafiri. Allaah akaita kuwa ni ufunguzi:

إِنَّا فَتَحْنَا لَكَ فَتْحًا مُّبِينًا

“Hakika Tumekupa ushindi ushindi wa wazi.” (al-Fath 48:01)

Pamoja na kuwa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alichukia hilo kwa sababu aliona kuwa ndani yake kuna ugumu kwa waislamu na kuwapa ushindi makafiri. Lakini yale aliyohukumu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio yenye kheri. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hazungumzi kwa matamanio yake mwenyewe. Hayakuwa ayatamkayo isipokuwa ni Wahy aliyofunuliwa. Kwa hivyo ni wajibu kuyatanguliza maneno ya Allaah na ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku zote na kwa hali zote. Usipingani au ukawa ndani ya moyo wako na uzito wowote kutokana na hayo. Ama ukiyachukia basi unaritadi. Tunamuomba Allaah afya.

[1] al-Bukhaariy (4189) na Muslim (1785).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 121-123
  • Imechapishwa: 06/12/2018