Swali 93: Je, kuna uwezekano watu wakawa na umoja pamoja na kutofautiana kwa mifumo na ´Aqiydah?

Jibu: Haiwezekani kukusanyika pamoja na kutofautiana kwa mifumo na ´Aqiydah.  Ushahidi mzuri wa hilo ni hali ya waarabu kabla ya kutumilizwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walikuwa wamegawanyika na daima wenye magomvi. Wakati walipoingia katika Uislamu na wakawa wamoja katika kumwabudu Allaah pekee, ´Aqiydah moja na mfumo mmoja, ndipo wakawa na umoja na dola yao ikasimama. Allaah (Ta´ala) amewakumbusha jambo hilo pale aliposema:

وَاذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ كُنتُمْ أَعْدَاءً فَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِكُمْ فَأَصْبَحْتُم بِنِعْمَتِهِ إِخْوَانًا

”Kumbukeni neema ya Allaah juu yenu, pale mlipokuwa maadui, kisha akaunganisha nyoyo zenu, mkawa kwa neema Yake ndugu.”[1]

Amesema (Ta´ala) kumwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

لَوْ أَنفَقْتَ مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا مَّا أَلَّفْتَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ أَلَّفَ بَيْنَهُمْ ۚ إِنَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

”Lau ungelitoa vyote vilivyomo ardhini, basi usingeliweza kuunganisha kati ya nyoyo zao, lakini Allaah amewaunganisha. Hakika Yeye ni Mwenye nguvu Asiyeshindika, Mwenye hekima ya yote.”[2]

Allaah (Subhaanah) kamwe hafanyi nyoyo za makafiri, walioritadi na mapote potofu kukusanyika[3]; Allaah huziunganisha nyoyo za waumini na wapwekeshaji. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu makafiri, wanafiki na wale wanaoenda kinyume na mfumo na ´Aqiydah ya Uislamu:

تَحْسَبُهُمْ جَمِيعًا وَقُلُوبُهُمْ شَتَّىٰ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَعْقِلُونَ

”Utawadhania wameungana pamoja, kumbe nyoyo zao zimetengana. Hayo ni kwa sababu wao ni watu wasiotia akilini.”[4]

وَلَا يَزَالُونَ مُخْتَلِفِينَ إِلَّا مَن رَّحِمَ رَبُّكَ

“Na hawatoacha kuendelea kutofautiana. Isipokuwa yule aliyemrehemu Mola wako.”[5]

Nao ni wale watu wenye ´Aqiydah na mfumo sahihi; hao ndio ambao husalimika kutokamana na tofauti.

Kwa hivyo wale wanaojaribu kuwakusanya watu licha ya kuharibika ´Aqiydah na kutofautiana kwa mifumo yao wanajaribu jambo lisilowezekana kabisa. Kwani ni muhali kabisa kukusanya kati ya vinyume viwili. Hakuna kinachoziunganisha nyoyo za watu na kuleta umoja isipokuwa Tawhiyd[6], kwa sharti ijulikane maana ya Tawhiyd na muqtadha yake ikafanyiwa kazi kwa nje na kwa ndani. Sio kuitamka na wakati huohuo mtu akaenda kinyume na yale inayofahamisha. Hapo haitofaa kitu.

[1] 3:103

[2] 8:63

[3] Dalili kubwa ya hilo ni yale mapote na makundi yaliyopo hii leo. Ni wenye kutofautiana juu ya Kitabu na wanaenda kinyume na Qur-aan. Mioyo inapoafikiana na kufahamiana huungana, na si kinyume chake. Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Roho ni wanajeshi walioshikana. Wale ambao wataafikiana wataungana na wale ambao hawatoafikiana watatengan.” (al-Bukhaariy (3158))

[4] 59:14

[5] 11:118-119

[6] Mfano wa ambao wanajaribu kuwakusanya watu licha ya kuharibika kwa ´Aqiydah na kutofautiana kwa mifumo leo hii ni al-Ikhwaan al-Muslimuun ambayo imebeba Raafidhwah, Jahmiyyah, Ashaa´irah, Khawaarij, Mu´tazilah na mkristo. Katika kitabu hichi umekwishasoma yale yaliyosemwa na wanazuoni kuhusu al-Ikhwaan al-Muslimuun ya kwamba hawaipi umuhimu Tawhiyd wala hawatahadharishi shirki. Sifa hii ni alama pia kwa kipote cha Jamaa´at-ut-Tabliygh, na wala al-Ikhwaan al-Muslimuun na Qutbiyyah hawako mbali nayo.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 225-227
  • Imechapishwa: 05/08/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy