Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Imani ni kutamka kwa ulimi, kutakasa kwa moyo na matendo ya viungo. Inazidi kwa kuongezeka matendo mema na inashuka kwa kupungua matendo mema. Kwa hiyo ni yenye kupungua na kuongezeka.

MAELEZO

Miongon mwa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kwamba imani ni kutamka kwa ulimi, kuamini kwa moyo na vitendo vya mwili, inazidi kwa utiifu na inapungua kwa maasi. Namna hii ndivo Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaifasiri imani.

Kutamka kwa ulimi kumekusanya shahaadah, kumtaja Allah, Tasbiyh, Tahlyl, kuamrisha mema, kukataza maovu, mafunzo na matendo mengine ya kimaneno. Ni matendo mengi, lakini hayatoshi. Kwa sababu wanafiki husema:

آمَنَّا بِاللَّـهِ وَبِالرَّسُولِ وَأَطَعْنَا ثُمَّ يَتَوَلَّىٰ فَرِيقٌ مِّنْهُم مِّن بَعْدِ ذَٰلِكَ ۚ وَمَا أُولَـٰئِكَ بِالْمُؤْمِنِينَ

”Tumemwamini Allaah na Mtume na tumetii. Kisha hugeuka kundi katika wao baada ya hayo – na wala hao si wenye kuamini.”[1]

Kwa hivyo imani sio kutamka kwa ulimi peke yake.

Imani sio kuamini kwa moyo peke yake kama wanavosema Murji-ah. Ni maoni batili. Mambo yangelikuwa hivo basi makafiri wangelikuwa waumini. Kwa sababu wanaamini ndani ya mioyo yao kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Mtume wa Allaah. Hata hivyo kiburi, hasadi na mori za kipindi cha kikafiri za kuwafuata mababu zao ndio yaliyowazuia kumfuata. Amesema (Ta´ala):

قَدْ نَعْلَمُ إِنَّهُ لَيَحْزُنُكَ الَّذِي يَقُولُونَ ۖ فَإِنَّهُمْ لَا يُكَذِّبُونَكَ وَلَـٰكِنَّ الظَّالِمِينَ بِآيَاتِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ

“Hakika tunajua kwamba yanakuhuzunisha yale wanayoyasema. Hakika wao hawakukadhibishi wewe lakini madhalimu wanakanusha alama za Allaah.”[2]

Imani sio kuamini kwa moyo peke yake. Ni lazima yapatikane matendo. Kama mfano wa swalah, zakaah, kuhiji na matendo mengine yote mema. Amesema (Ta´ala):

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا

“Hakika si venginevyo waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah, basi nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayah Zake huwazidishia imani na kwa Mola wao wanategemea; ambao wanasimamisha swalah na hutoa sehemu katika yale tuliyowaruzuku. Hao ndio Waumini wa kweli!  Wana ngazi [za juu] kwa Mola wao na msamaha na riziki tukufu.”[3]

Ametaja pia matendo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Imani ni tanzu sabini na kitu. Ya juu yake ni “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” na ya chini yake ni kuondosha chenye kuudhi njiani. Hayaa pia ni tanzu katika imani.”[4]

Hadiyth imefahamisha kwamba imani ni kutamka kwa ulimi, nako ni kule:

“Ya juu yake ni “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”.”

Vivyo hivyo Adhkaar nyenginezo zilizowekwa katika Shari´ah. Shahaadah ndio tanzu yake ya juu kabisa. Tanzu yake ya chini ni:

“… kuondosha chenye kuudhi njiani.”

Ni kitendo chema. Ingawa ni kidogo lakini ni katika imani. Hayaa inayomzuia mtu kutokamana na mambo yasiyokuwa ya sawa, maasi, machafu na tabia mbaya ni katika imani. Hayaa kama hiyo ni yenye kusifiwa na ni sehemu katika imani. Imekuja katika Hadiyth:

“Hayaa ni sehemu katika imani.”

Ni dalili inayojulisha kuwa imani imegawanyika sehemu mbalimbali na sio kitu kimoja. Ni sehemu nyingi. Matendo yote mema ni katika tanzu za imani.

[1] 24:47

[2] 06:33

[3] 8:2-4

[4] al-Bukhaariy (9) na Muslim (35).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 70-71
  • Imechapishwa: 25/08/2021