Itambulike kuwa moto na ule umanjano ndani ya kaburi sio kama moto na umanjano wa duniani. Ni katika moto na umanjano wa Aakhirah. Ni wenye kuumiza na mkali zaidi kuliko umanjano na moto wa hapa duniani. Allaah akimhukumu mtu adhabu basi unatiwa moto ule udongo wake, mawe au kokote zilizo juu yake na chini yake ndani ya kaburi mpaka inakuwa na moto zaidi kuliko kaa la moto la duniani. Lau watu wataligusa ardhi hawatohisi kitu. Hawaoni kitu zaidi ya udongo, mawe na kokoto. Bali watu wawili wanaweza kuzikwa kwenye kaburi moja ambapo mmoja wao akawa katika shimo miongoni mwa mashimo ya Motoni na mwingine akawa katika bustani miongoni mwa mabustani ya Peponi. Moto wa mmoja wao haumfikii mwingine na neema anazoneemeka mmoja wao hazimfikii mwingine. Uwezo wa Allaah ni mpana, wenye kukata kabisa na wa ajabu kuliko hivo! Yote haya yanapitika ili waumini waweze kuwa na bidii na kumwogopa Allaah (Ta´ala) zaidi. Wanatakiwa kutambua kuwa Allaah anawachunga katika hali ya siri na hadharani. Yanapelekea kuzidi kujichumia thawabu nyingi. Tuliyoyataja ni katika kuamini mambo yaliyofichikana. Muumini anatakiwa kujua kuwa mbele yake kuna hali na vikwazo vinavyomsubiri – tunamuomba Allaah usalama.

Hata kama haya tuliyoyataja ni katika elimu ya mambo yaliyojificha Allaah (´Azza wa Jall) anaweza kumfunulia yule Anayemtaka kutokana na ajabu ya uwezo Wake. al-Bukhaariy amepokea kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Lau msingelikufa basi ningemuomba Allaah aweze kuwasikilizisha yale ninayoyasikia katika adhabu ya kaburi.”

al-Bukhaariy amepokea vilevile kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipita karibu na makaburi mawili na akasema:

“Hawa wanaadhibiwa na hawaadhibiwi kwa kitu kikubwa.”

´Allaamah Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema katika kitabu chake “ar-Ruuh”:

“Mwenzetu Abu ´Abdillaah Muhammad bin al-Waziyr al-Harraaniy alinieleza ya kwamba siku moja alitoka nyumbani baada ya ´Aswr na kusema: “Pindi jua lilipozama nikasimama katikati ya makaburi. Nikaona kaburi lililo na kaa la moto kama kioo yazua. Katikati ya kaburi alikuwepo maiti. Nikaanza kujifuta macho yangu na kufikiria: “Hivi kweli naota au niko macho?” Kisha nikageuka na kuona ukuta wa mji. Nikasema: “Ninaapa kwa Allaah sioti.” Nikaenda nyumbani kwa familia yangu katika hali ya kuchanganyikiwa. Wakanipa chakula, lakini sikuweza kula. Halafu nikaenda mjini na kuuliza juu ya mwanaume wa kaburi lile. Wakasema kwamba alikuwa ni afisa mmoja wa forodha aliyekufa siku ileile.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 202-203
  • Imechapishwa: 04/12/2016