´Abdullaah bin Abiyl-Hudhayl amesema:

”Hakika Allaah (Ta´ala) anapenda atajwe sokoni na anapenda atajwe katika kila hali – isipokuwa katika choo.”

Inatosha katika hali hiyo kuwa na hisia ya haya, uangalizi na kutambua neema ya Allaah katika hali hiyo, nayo ni katika aina kuu za Dhikr. Basi Dhikr ya kila hali huwa kwa mujibu wa inavyostahiki hali hiyo. Inavyostahiki hali hii ni kujifunika kwa vazi la haya mbele ya Allaah (Ta´ala), kumtukuza, kumkumbuka kwa neema Yake na wema Wake kwa kumwezesha mtu kutoa adui huyu mwenye kuumiza ambaye lau angesalia tumboni basi angemuua. Basi neema ya kurahisishiwa kutoka kwake ni sawa na neema ya kula kwake awali. ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa anapotoka chooni anapapasa tumbo lake na kusema:

“Enyi watu, Ni ni iliyoje hii, lau watu wangelijua thamani yake!”

Baadhi ya Salaf walikuwa wakisema:

“Himdi zote njema anastahiki Allaah, ambaye amenionjesha ladha yake, akaacha ndani yangu manufaa yake na akaondoa kwangu madhara yake.”

Kama hayo yanaweza kusemwa kuhusu Dhikr wakati wa jimaa, ambayo ndio neema kubwa zaidi ya ulimwenguni. Akimtaja Allaah (Ta´ala) kwa neema hii aliyopewa, basi moyo wake unachochewa na msukumo wa shukurani. Kwani Dhikr ni kichwa cha shukurani. Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anh) amesinulia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimshika mkono na akamwambia:

“Naapa kwa Allaah, ee Mu´aadh, nakupenda. Basi usiache kusema baada ya kila swalah:

اللَّهُمَّ أَعِنِّي على ذِكْرِكَ وَشُكْرِكَ وَحُسْنِ عِبَادَتِكَ

”Ee Allaah! Nisaidie kukutaja, kukushukuru na kufanya vizuri ´ibaadah Yako.”[1]

Akakusanya kati ya Dhikr na kushukuru, kama Alivyokusanya (Subhanaahu wa Ta´ala) pale aliposema:

فَاذْكُرُونِي أَذْكُرْكُمْ وَاشْكُرُوا لِي وَلَا تَكْفُرُونِ

“Basi nidhukuruni na Mimi nitakukumbukeni na nishukuruni wala msinikufuru!”[2]

Kwa hivyo kufanya Dhikr na kushukuru ndio msingi wa furaha na mafanikio.

[1] Abu Daawuud (1517), an-Nasaa’iy (1302), Ahmad (7/380), Ibn Khuzaymah (751), Ibn Hibbaan (2020) na al-Haakim (1/273), ambaye ameisahihisha.

[2] 2:152

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 163
  • Imechapishwa: 04/09/2025