Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Mashairi ya Umayyah bin Abiys-Swalt yaliyokubaliwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alisema:

Mtukuze Allaah, na hakika ni Mwenye kustahiki kutukuzwa

Mola wetu Yuko juu ya mbingu, jioni imefika

kwa jengo kubwa ambalo limetangulia viumbe

Ameumba ´Arshi juu ya mbingu 

Macho hayawezi kuitazama

chini yake wako Malaika wanaotazama juu

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Mashairi yake yameamini ilihali moyo wake umekufuru.”[1]

MAELEZO

Umayyah bin Abiys-Swalt alikuwa ni miongoni mwa washairi wa kipindi kabla ya kuja Uislamu. Alikuwa ni mnaswara mfanya ´ibaadah anayefikiria kuwa yeye ndiye ambaye atakuja kuwa Nabii na akawa anajibidisha kwelikweli kuutafuta huo unabii. Wakati alipotumilizwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akamuhusudu na kumkufuru. Lakini wakati mwingine katika kipindi kabla ya kuja Uislamu alikuwa akisoma mashairi ambayo ndani yake kuna haki, kukiwemo misitari hii iliyotajwa. Jengine ni kwamba utume haupatikani kwa uzoefu au bidii; utume ni chaguo na uteuzi kutoka kwa Allaah. Yeye (´Azza wa Jall) ndiye anayechagua. Amesema (Ta´ala):

اللَّـهُ أَعْلَمُ حَيْثُ يَجْعَلُ رِسَالَتَهُ

“Allaah anajua zaidi wapi aweke ujumbe Wake.”[2]

اللَّـهُ يَصْطَفِي مِنَ الْمَلَائِكَةِ رُسُلًا وَمِنَ النَّاسِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ بَصِيرٌ

“Allaah anateua wajumbe miongoni mwa Malaika na miongoni mwa watu. Hakika Allaah ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[3]

Utume haupatikani kwa uzoefu au kwa kuilea nafsi. Utume ni fadhilah kutoka kwa Allaah, na Allaah anamchagua yule ambaye anajua kuwa anafaa zaidi juu ya utume:

وَإِذَا جَاءَتْهُمْ آيَةٌ قَالُوا لَن نُّؤْمِنَ حَتَّىٰ نُؤْتَىٰ مِثْلَ مَا أُوتِيَ رُسُلُ اللَّـهِ ۘ اللَّـهُ أَعْلَمُ حَيْثُ يَجْعَلُ رِسَالَتَهُ

”Na inapowajia alama, basi husema ”Hatutoamini mpaka tupewe mfano wa yale waliopewa Mtume wa Allaah” – Allaah anajua zaidi wapi aweke Ujumbe Wake.”[4]

Umayyah bin Abiys-Swalt hakukipata kile ambacho alikuwa anajipindisha kukitafuta ambapo akamuhusudu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mashairi yake yameamini ilihali moyo wake umekufuru.”

Kwa sababu amesema haki, lakini moyo wake umekufuru kwa sababu hakumuamini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokana na hasadi yake na akamkasirikia Allaah kwa vile hakumteua yeye kuwa Mtume.

Kinachokusudiwa katika mashairi yake ni maneno yake “Mola wetu Yuko juu ya mbingu”.  Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamkubalia hilo. Hii ni dalili inayofahamisha kuwa watu katika kipindi kabla ya kuja Uislamu walikuwa wakithibitisha kuwepo juu kwa Allaah.

[1] adh-Dhahabiy amesema:

”Cheni ya wapokezi imekatika.” (al-´Uluww, uk. 50)

[2] 6:124

[3] 22:75

[4] 6:124

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 131-132
  • Imechapishwa: 27/08/2024