87- Ni lazima kumzika maiti hata kama ni kafiri. Kumepokelewa Hadiyth mbili kuhusiana na hilo:

Ya kwanza: Kutoka kwa kikosi cha Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), miongoni mwao ni Abu Twalhah al-Answaariy, na mtiririko ni wake:

“Kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoa amri siku ya Badr juu ya watu ishirini na nne katika viongozi wa Quraysh. [Wakaburuzwa kwa miguu yao] wakatupwa ndani ya kisima miongoni mwa visima vya Badr kibaya na kikazidi ubaya [wakiwa wamepandiana baadhi juu ya wengine], [isipokuwa kwa yale yaliyomtokea Umayyah bin Khalaf; yeye alivimba ndani ya nguo yake ambapo akajaa. Wakaenda kutaka kumkokota akawa anakatikakatika viungo. Wakamwacha na wakammiminia mawe na udongo vitavyomfunika]. Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapowashinda watu basi hukaa katika ule uwanja wa vita kwa muda wa siku tatu. Alipokuwa katika Badr ile siku ya tatu aliamrisha awekewe juu ya kipando chake kile kibanda chake. Kisha akaondoa na Maswahabah zake wakamfuata. Wakasema: “Tunaona kuwa anaondoka kukidh baadhi ya haja zake mpaka aliposimama juu ya mdomo wa kile kisima. Akawa anawaita kwa majina yao na majina ya baba zao [ilihali wamekwishakuwa mizoga] : [Ee Abu Jahl bin Hishaam! Ee ´Utbah bin Rabiy´ah! Ee Shaybah bin Rabiy´ah! Ee Waliyd bin ´Utbah!] Je, hakukufurahisheni jambo la nyinyi endapo mgelikuwa mumemtii Allaah na Mtume Wake? Hakika sisi tumekuta yale aliyotuahidi Mola Wetu ni haki. Je, nyinyi mmekuta yale mliyoahidiwa na Mola Wenu ni haki?” [´Umar akayasikia maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)] Akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni vipi unazungumzisha miili ya isiyokuwa na roho. [Je, wanasikia? Allaah (´Azza wa Jall) anasema:

إِنَّكَ لَا تُسْمِعُ الْمَوْتَىٰ

“Hakika wewe huwezi kusikilizisha wafu.”[1]]

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi Mwake kwamba nyinyi hamsikii vyema kuliko wao. [Ninaapa kwa Allaah] [wao hivi sasa wanajua kwamba yale niliyokuwa nawaambia ndio ya haki] Katika upokezi mwingine imekuja: “Wao hivi sasa wanasikia [zaidi ya kwamba hawana uwezo wa kunijibu chochote]. Qataadah amesema: “Allaah  amewapa uhai [kwa ajili yake] mpaka akawasikilizisha maneno yake kwa ajili ya kuwabeza, kuwadogesha, malipo ya adhabu na kuwaonyesha majuto.”

Wameipokea kikosi cha Maswahabah na huu ni upokezi wa baadhi yao ambao ni:

1- Abu Twalhah al-Answaariy. Ameipokea Qataadah na akasema: “Ametutajia nayo Anas bin Maalik kutoka kwa Abu Twalhah.”

Ameipokea al-Bukhaariy (07/240-241) na tamko ni lake, Muslim (08/164), Ahmad (04/129) na ziada ya tano ni yake na iko kwa mujibu wa sharti za Muslim. Pia ameipokea an-Nasaa´iy (01/293). Lakini katika cheni ya wapokezi wake hakumtaja Abu Twalhah, nao ni upokezi wa Muslim (08/163), Ahmad (03/104, 145, 182, 219-287) na yeye ndiye mwenye ziada ya kwanza na ya saba. Cheni za wapokezi wawili hao ni Swahiyh juu ya sharti za Muslim. Watatu hao ndio wenye ziada ya nne na ya tano isipokuwa wamesema: “Umayyah bin Khalaf” badala ya “Waliyd bin ´Utbah”. Ni kosa kutoka kwa baadhi ya wapokezi. Kwani Umayyah hakuwa kisimani, hivo ndivo inavojulisha ziada ya pili. Nayo iko katika Hadiyth ya ´Aaishah, kama itavokuja kwa cheni ya wapokezi nzuri. Kwao iko ziada ya sita na ya kumi na Ahmad anayo ziada ya kumi na moja.

2- ´Umar bin al-Khattwaab ambaye Anas amepokea pia mfano wake kutoka kwake. Juu yake kuna ziada ya pili. Ameipokea Muslim, an-Nasaa´iy na Ahmad (nambari. 182).

3- ´Abdullaah bin ´Umar. Anao upokezi wa pili. Juu yake kuna ziada ya tisa.

Ameipokea al-Bukhaariy (07/242-242-243), Ahmad (nambari. 4864, 4958, 6145) na katika upokezi wake imetajwa:

“Jambo hilo likatajwa kwa ´Aaishah ambapo akasema: “Hivi amesahau – bi maana Ibn ´Umar? –  Hakika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Hakika wao hivi sasa… “ Cheni ya wapokezi wake ni nzuri. Juu yake kuna ziada ya pili kama tulivotangulia kusema.

Tambua kwamba wanachuoni wameona kuwa upokezi wa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) ni wa sawa kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika wao hivi sasa wanasikia.”

na wakaraddi maneno yake:

“Hivi amesahau.”

kwa sababu yeye Ibn ´Umar ni mwenye kuthibitisha na yeye ´Aaishah ni mwenye kupinga. Jengine ni kwamba yeye Ibn ´Umar hakupwekeka kwa hilo. Bali kama ilivyotangulia baba yake ´Umar, Abu Twalhah na wengineo wamepokea mfano wake, kama ilivyo katika “al-Fath”. Rejea kama unataka upambanuzi zaidi. Haki ni kwamba yale yaliyopokelewa na kikosi cha wengi ndio ya sawa na vivyo hivyo yale aliyopokea ´Aaishah. Wote ni waaminifu. Wala hakuna mgongano kati ya mapokezi mawili. Hivyo moja itaoanishwa na nyingine, kama tulivofanya katika mtiririko wa Hadiyth.

Ameipokea Ahmad (06/276), Ibn Hishaam katika “as-Siyrah” (02/74) kwa cheni ya wapokezi nzuri. Juu yake kuna ziada ya tatu.

Ya pili: ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Wakati alipofariki Abu Twaalib nilimwendea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nikasema: “Hakika yule ami yako mzee [mpotofu] ameshakufa. [Ni nani atakayemfukia?] Akasema: “Nenda umfukie. Kisha usifanye lolote mpaka unijie. [Akasema: “Amekufa akiwa ni mshirikina[2]. Akasema: “Nenda umfukie[3]]. Nikamfukia kisha nikamjia. Akasema: “Nenda ukaoge kisha usifanye lolote mpaka utakaponijia.” Nikaoga kisha nikamwendea. Akasema: “Akaniombea du´aa nyingi zilizonifurahisha zaidi kuliko kupata ngamia wekundu na weusi wake.” Amesema: “´Aliy alikuwa anapomuosha maiti basi huoga.”

Ameipokea Ahmad (nambari. 807) na mtoto wake katika Zawaa-id “al-Musnad” (nambari. 1074) kupitia kwa ´Abdur-Rahmaan as-Sulamiy kutoka kwake.

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.

Ameipokea Abu Daawuud (02/70), an-Nasaa´iy (01/282-283), al-Bayhaqiy (03/398), Ahmad pia (nambari. 759) kupitia kwa Abu Ishaaq: Nimemsikia Naajiyah bin Ka´b akihadithia kutoka kwa ´Aliy mfano wake. Ziada ni za Ahmad isipokuwa ya pili ambayo ni ya an-Nasaa´iy.

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh pia. Wapokezi wake wote ni waaminifu. Ni wapokezi wa al-Bukhaariy na Muslim isipokuwa tu Naajiyah bin Ka´b. al-´Ijliy amesema katika “ath-Thiqaat”:

“Ni mtu wa Kuufah, ´Taabiy´ na ni mwaninifu.”

al-Haafidhw amesema katika “at-Taqriyb”:

“Mwaminifu.”

Kuhusu maneno aliyosema an-Nawawiy katika “al-Majmuu´” (05/181):

“Ameipokea Abu Daawuud na wengineo. Cheni ya wapokezi wake ni dhaifu.”

ni yenye kurudishwa na wala hatujui namna yake. Isipokuwa akiwa anakusudia kwamba ni katika mapokezi ya Abu Ishaaq, ambaye ni as-Sabiy´, ambaye alichanganyikiwa wakati alipokuwa mtumzima. Mambo yakiwa ni hivo, basi jibu ni kwa njia mbili:

1- Ni yenye kutokana na upokezi wa Sufyaan ath-Thawriy kutoka kwake, ambaye ni katika watu madhubuti juu yake. Hayo yametajwa katika “at-Tahdhiyb”.

2- Hakupwekeka nayo. Bali kama ilivyotangulia imekuja katika njia ya kwanza. Ni kama kwamba an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) hakuiona au hakuihudhurisha wakati alipozungumzia Hadiyth hii. Huenda ameegemea katika kuidhoofisha kwa al-Bayhaqiy. al-Haafidhw amesema katika “at-Talkhiysw”(05/149-150) baada ya kuiegemeza kwa Ahmad, Abu Daawuud, an-Nasaa´iy, Ibn Abiy Shaybah, Abu Ya´laa, al-Bazzaar na al-Bayhaqiy kupitia kwa Abu Ishaaq:

“Mzunguko mzima wa maneno ya al-Bayhaqiy ni kwamba ni dhaifu. Haibainiki namna ya udhaifu wake. ar-Raafiy´ amesema: “Ni Hadiyth imara na iliyotangaa. Amesema hayo katika “Amaalih” yake.”

Ameiegemeza katika “al-Fath” (07/154) ya Ibn Khuzaymah pia na Ibn-ul-Jaaruud.

Faida!

Hadiyth hii al-Bayhaqiy ameileta katika mlango “Muislamu anawaosha jamaa zake wa karibu katika washirikina, anasindikiza majeneza yao, anawazika na wala hawaswalii.”

Wewe unaona kwamba hakuna katika Hadiyth yale aliyoyawekea mlango kuhusu kuosha. al-Haafidhw amesema akiwa ni mwenye kuyatolea maelezo maneno yake:

“Uzindushi! Hakuna chochote katika njia ya Hadiyth hizi kusema wazi kwamba alimuosha. Isipokuwa ikiwa kama hayo yatachukuliwa katika maneno yake: “Akaniamrisha nikaoga.” Hakika kuoga ni jambo limesuniwa baada ya kumuosha maiti na wala halijasuniwa kwa ajili ya kumzika. al-Bayhaqiy na wengine hawakujenga hoja isipokuwa juu ya jambo la kumuosha baada ya kumuosha maiti. Imekuja kwa Abu Ya´laa kwa mtazamo mwingine mwishoni mwake:

“´Aliy alikuwa anapomuosha maiti basi huoga.”

Kama tulivotangulia kusema ziada hii iko kwa Ahmad pia na mtoto wake. Inashangaza ni vipi jambo hilo lilifichikana kwa al-Haafidhw na khaswa kwa kuzingatia kwamba ameiegemeza Hadiyth kwa Ahmad, kama ulivyojionea mwenyewe.

Jengine ni kwamba maneno yake:

“… na wala halijasuniwa kwa ajili ya kumzika.”

ni jambo linahitaji kujadiliwa. Kwa sababu huenda mtu akasema: “Hadiyth ina dalili ya wazi juu ya usuniwaji wa jambo hilo. Halipingani na ziada iliyojitokeza mwishoni mwa Hadiyth. Kwa sababu ni jumla yenye kujitegemea. Haina mafungamano yoyote na yaliyo kabla yake. Ninachokusudia ni kwamba katika Hadiyth hakuna dalili kwamba ´Aliy alikuwa akioga baada ya kumuosha maiti eti kwa ajili tu ya kumwamrisha kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuoga katika Hadiyth. Bali hili ni jambo moja na lile ni jambo lingine. Ni kweli kwamba ikiwa upokezi ufuatao utathibiti basi hakuna budi isipokuwa kusalimu amri kutokana na yaliyothibiti kwa al-Haafidhw. Amesema punde tu baada ya maneno yake aliyoyataja:

“Nimesema: “Imetajwa kwa Ibn Abiy Shaybah katika “Muswannaf” yake kwa tamko: “Nikasema: “Hakika ami yako mzee kafiri amekufa. Unasemaje juu yake?” Akasema: “Naona umuoshe na umsitiri.”

Imepokelewa katika njia nyingine kwamba alimuosha. Ameipokea Ibn Sa´d kutoka kwa al-Waaqidiy.”

Huyu al-Waaqidiy ni mwenye kuachwa. Anatuhumuwa wongo. Hivyo ziada yake haina maana yoyote. Ama kuhusu ziada ya Ibn Abiy Shaybah:

“Naona umuoshe.”

ni mbovu pia. Kwa sababu ameitoa (04/142) kutoka katika njia ya al-Ajlah kutoka kwa Sha´biy ikiwa ni cheni isiyokuwa Swahabah. Pamoja na kuwa kwake hivo, al-Ajlah mwenyewe ana unyonge. Kwa hivyo yeye pia hakuna hoja juu ya ziada yake.

[1] 27:80

[2] Maneno haya yako wazi juu ya kwamba Abu Twaalib alikufa akiwa ni kafiri mshirikina. Zipo Hadiyth nyingi kuhusiana na maudhui haya. Miongoni mwazo ni Hadiyth ya Ibn Hazm iliyokwishatangulia katika masuala ya 60. al-Haafidhw amesema akiwa ni mwenye kuitolea maelezo:

“Nimeona kijimakala kilichokusanywa na mmoja katika Raafidhwah ambaye ametaja kwa wingi Hadiyth mbovu zinazofahamisha juu ya Uislamu wa Abu Twaalib. Hakuna chochote katika hizo iliyothibiti. Tawfiyq inaombwa kutoka kwa Allaah. Nimeyafupiza hayo katika wasifu wa Abu Twaalib katika kitabu “al-Iswaabah”.”

[3] Miongoni mwa makosa katika Hadiyth hii ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumpa pole ´Aliy kwa kufariki kwa baba yake mshirikina. Pengine ikawa ni dalili inayofaa kutumiwa kwa kutokukubalika Kishari´ah kumpa pole muislamu kwa kufiliwa na ndugu yake ambaye ni kafiri. Ni jambo lina haki zaidi kuwa dalili ya kutokufaa kuwapa pole makafiri kwa kufiliwa na wafu wao asilani.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 167-172
  • Imechapishwa: 16/02/2022